BAADA ya kuinyoosha Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara
mwishoni mwa wiki, Yanga leo inaingia kambini kujiandaa na mechi mbili,
imeelezwa.
Kesho Jumatano, Yanga ambao ni mabingwa wa
Tanzania Bara, watacheza
na JKT Mlale katika mchezo wa Kombe la FA kwenye Uwanja wa Taifa jijini
Dar es Salaam huku Jumamosi wakiwa na kibarua dhidi ya timu ya Mauritius
ya Cercle de Joachim.
Katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika uliopigwa
Mauritius mwishoni mwa wiki iliyopita, Yanga iliibuka na ushindi wa bao
1-0 na hivyo kuhitaji sare au ushindi wa aina yoyote ili kusonga mbele.
Yanga inacheza mechi hizo mbili ikiwa iko vizuri baada ya Jumamosi
kuwafunga watani zao wa jadi Simba kwa kuwafunga mabao 2-0 katika mchezo
wa Ligi Kuu Tanzania Bara ulioirejesha timu hiyo kileleni mwa msimamo
wa ligi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam Mkuu wa Idara
ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema kikosi hicho
kitaweka kambi yake jijini.
“Tunashukuru Mungu tulimaliza mchezo wetu na Simba salama kwa kupata
ushindi mzuri, kikosi kimeanza mazoezi leo (jana) kwenye uwanja wa Chuo
cha Polisi Kurasini na kesho(leo) kitaingia kambini kujiandaa na michezo
ijayo,” alisema.
Muro alisema wamejiandaa kufanya vizuri katika mchezo huo ili
kutimiza malengo waliyojiwekea ya kufika hatua ya makundi. Katika hatua
nyingine, uongozi wa Yanga umewapongeza wachezaji na benchi nzima la
ufundi kwa kufanya vizuri katika mchezo uliopita dhidi ya Simba na
kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
“Uongozi wa Yanga unawapongeza wachezaji na kuwashukuru benchi la
ufundi kwa kufanya kazi nzuri ile waliyotumwa, ni kazi waliyopewa na
taifa la Watanzania, lakini pia tunawapongeza wanachama, mashabiki na
wapenzi waliounga mkono timu,” alisema.
Muro alisema kwenye suala la Ligi Kuu wamefunga ukurasa na watani wao
Simba na kwamba sasa sio wapinzani wao bali wamebaki kuwa watani wao wa
jadi.
0 comments:
Post a Comment