Wednesday, 24 February 2016

Umeme wa uhakika utachochea uchumi

SERIKALI kwa muda sasa imekuwa ikitoa mwito kwa watu wenye uwezo wa ndani na nje kuwekeza katika sekta ya nishati kwa lengo la kuwezesha taifa kuwa na umeme wa kutosheleza mahitaji
wakati likielekea kuwa taifa la viwanda na kipato cha kati.
Miongoni mwa maeneo ya kipaumbele yatakayoanza kutekelezwa katika bajeti ijayo ya mwaka wa fedha 2016/2017 ni kujenga uchumi wa viwanda kwa kutumia malighafi zinazopatikana nchini ikiwemo mazao ya misitu, kilimo, uvuvi na madini. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango anasema nia ya serikali ni kuvirudisha viwanda vilivyobinafsishwa na kutafuta wabia ambao wanaweza kufanyakazi iliyodhamiriwa.
Dk Mpango aliongeza kuwa ujenzi wa kiwanda cha chuma kwa kutumia malighafi inayozalishwa kwa kutumia chuma kutoka Liganga na Mchuchuma itakuwa ni msingi wa viwanda mama kwa kuwa hakuna ujenzi usiohitaji chuma. Anasema Serikali imedhamiria kushirikiana na sekta binafsi kwa kuwa maendeleo ya viwanda yanapaswa kuendana na maendeleo ya watu kwa kuwapatia ajira, elimu inayoendana na mahitaji ya viwanda ili maisha ya wananchi yawe bora zaidi.
Juhudi hizo za kufufua viwanda na kuanzishwa kwa viwanda vipya zinatakiwa kwenda sambamba na upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa bei nafuu ili viwanda hivyo viweze kujiendesha.
Uzalishaji umeme
Tanzania inategemea zaidi umeme unaozalishwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) japo wapo wazalishaji binafsi nje na ndani ya gridi ya taifa kwa mapatano na Tanesco. Huku kukiwa na mabadiliko makubwa ya tabia nchi, mfumo wa uzalishaji umeme kwa sehemu kubwa unategemea maji na kiasi kidogo ni ule unaotokana na mitambo inayoendeshwa kwa mafuta na gesi. Taarifa za Tanesco zinaonesha kuwa miaka minne iliyopita, umeme unaotokana na maji ulikuwa ni asilimia 57 ya umeme wote uliozalishwa na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Mchango wa gesi na mafuta
Katika kipindi cha mwaka 2012 uniti zilizozalishwa na kuingizwa ndani na nje ya gridi zilikuwa 5,759,756,313 huku Tanesco pekee ikizalisha uniti 3,110,436,062. Kwa mwaka huo wazalishaji binafsi na ule ulioagizwa kutoka Uganda na Zambia ulikuwa ni uniti 2,649,320,551. Kwa taifa linalotegemea umeme kujiondoa katika umasikini na kujiingiza katika dunia ya viwanda, kiwango hicho ni kidogo na hasa ukizingatia kwamba utegemezi wa maji katika mazingira ya tabia nchi yanayobadilika ni hatari kwa usalama wa upatikanaji wa nishati na bei bora.
Ingawa bwawa la Kidatu linaweza kuzalisha megawati 204 ;Kihansi megawati 180 ;Mtera megawati 80 ; Pangani megawati 68 ;Hale megawati 21 ;Nyumba ya Mungu megawati 8 na Uwemba megawati 0.82 na hivyo kuwa na jumla ya megawati 561 za umeme wa maji, kiwango hicho kimekuwa kikishuka kutokana na mabwawa mengi kukosa maji ya kutosha kuzalisha umeme na wakati mwingine kufungwa.
Kutokana na tatizo la maji katika miaka ya karibuni Tanesco ililazimika kuwa na umeme kwenye gridi unaotokana na mafuta na gesi kwa kutumia mitambo yake na mingine ya watu binafsi. Kwa kutumia mitambo yake inayoendeshwa kwa gesi iliyopo Dar es Salaam maeneo ya Ubungo inayozalisha megawati 100,Tegeta megawati 45, Tanesco imekuwa ikipumua kwa namna yake ingawa bado kunaendelea kuwapo na shida ya umeme wa kutosha.
Ingawa inaeleweka kuwa uzalishaji wa baadaye unategemea sana makaa ya mawe na gesi, Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospter Muhongo anasema ipo haja kubwa ya kuongeza vyanzo vya ufuaji umeme na hivyo kuwakaribisha wawekezaji. Waziri huyo anasema ni muhimu kama wazalishaji wadogo wakaongezewa nguvu ili umeme wa uhakika uzalishwe kwa ajili ya matumizi ya majumbani na viwandani.
Uzoefu kutoka nchi nyingine
Muhongo anasema nchi zenye uchumi mkubwa kama Marekani, China Japan na Ujerumani ziliendelea kutokana na kuwa na viwanda. “China imekuwa ya pili katika ukuaji wa uchumi wake kwa sababu uchumi wake ulikuwa unakua kwa asilimia 10 hadi 13, ndio maana upatikanaji wa umeme wa uhakika ni suala la lazima tena wa bei nafuu,” anasema Muhongo.
Anasema kupungua kwa bei ya umeme ni jambo la lazima si hiari na umeme huo lazima uwe wa uhakika na sio wa kubahatisha, kama ilivyo kwa sasa hapa nchini . Waziri Muhongo anasema umeme unaozalishwa nchini kwa sasa hauvuki megawati 1,500 hivyo juhudi lazima zifanyike kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo vingine.
Anavitaja vyanzo hivyo kama vya nguvu ya jua, mabaki ya miwa, mkonge, kuzalisha umeme kwa kutumia taka za aina mbalimbali na mimea na taka zinazojaa chini ya miti na hata unaotokana na joto la miamba. Akizungumzia uwezekano wa kupata umeme zaidi Profesa Muhongo anasema ipo haja ya kutumia vyanzo vingine ambavyo vimeonesha dalili na moja ya chanzo hicho ni umeme jua.
Athari za mabadiliko ya tabia nchi
Uzalishaji wa umeme kwa maji umezidi kushuka na shukrani kubwa ni kupatikana kwa gesi kwa wingi ambayo sasa ndio imechukua nafasi ya umeme wa maji.
Kwa mujibu wa Profesa Muhongo kwa sasa Tanzania chanzo cha kwanza cha umeme ni gesi inayotoa asilimia 50, asilimia 35 unaozalishwa kwa maji huku umeme wa mafuta ukiwa ni asilimia 15. Anasema katika mazungumzo yake kwa sasa taifa linahitaji kuachana na umeme wa mafuta kwani gharama zake ni kubwa.”Umeme huu unatakiwa kutumika wakati tu kama kuna ulazima…”.
“Umeme tunaouhitaji unatakiwa utufikishe kwenye Power Per Capital ….kama tunalipenda taifa letu miaka 10 ijayo tujitahidi tuwe na megawati 10,000 hadi 13,000 bila hivyo tutakuwa tunajichanganyachanganya… kama Tanesco hawana mwelekeo wa kuzalisha umeme mwingi lazima tuwe na Tanesco mpya bila hivyo hatuwezi kutoka kwenye umasikini tunataka uchumi ukue kutoka asilimia saba hadi asilimia 10,” anasema Muhongo.
Pia anasema wazalisha umeme wana haki ya kumuuzia umeme wanaozalisha mtu yeyote pasipo kupitia Tanesco. “Tanesco lazima wabadilike shirika hili lipo tangu miaka ya 1930 wakati wa wakoloni walikuwa wakijishughulisha na umeme wa maji na wakati huo kutokana na uchache wa watu umeme ulikuwa unatosheleza, wakalala usingizi wote tukajikuta tumelala usingizi wa pono,” anasema Muhongo.
Ingawa serikali imeachia watu wenye uwezo kujitokeza kusaidia juhudi za kupata umeme zaidi na kama Tanesco haiwezi itabidi kuwapo na vyanzo vingine, kuna dalili nzuri za kuzalisha umeme kutokana na joto la ardhi kutokana na utafiti unaofanywa katika eneo la mto Ngozi uliopo mkoani Mbeya. “Tunatafuta mwekezaji wa Umeme joto wazalishe kwenye bonde la ufa megawati 15,000,” anasema Muhongo.
Anasema katika juhudi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kukuza uchumi kutoka asilimia saba hadi asilimia 10, lazima kuwepo umeme wa kutosha ili kuhudumia viwanda pamoja na watu ambao wanatarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2025. Profesa Muhongo anabainisha kuwa, mwaka 2012 wakati wa Sensa ya Watu na Makazi, Tanzania ilikuwa na watu milioni 45 na mwaka huu inakadiriwa kuongezeka kufikia milioni 53.5.
Kwani umeme wetu ni kidogo?
“Umeme uliopo hautoshi na inakadiriwa ifikapo mwaka 2025 tutakuwa watu milioni 80 umeme hautatosha, pato letu la mtu mmoja mmoja ni dola 998 ili tuwe nchi ya kipato cha kati pato la kila moja liwe dola 3,000 sasa GDP ipo dola 55 bilioni, tukiwa milioni 80 GDP lazima iwe dola milioni 200,” alisema Muhongo. Kwa maelezo ya Waziri na wataalamu wengine kazi iliyopo ni kutoka katika pato hilo la dola bilioni 55 na hilo litawezekana kama umeme utakuwa wa kutosha.
“Umeme wote tulionao tukiuweka pamoja hatuvuki megawati 1,500 ni umeme kidogo tunahitaji umeme zaidi,” alisisitiza. Aidha umeme unaozalishwa ukigawa kwa Watanzania wote ni uniti 108 kwa mwaka na ukigawa kwa 12 kila mtu anapata uniti tisa kwa mwezi, hiyo inaeleza jinsi tulivyo masikini. Pia kama Tanzania inataka kufikia uchumi wa kati ni lazima izalishe umeme wa kutosha kwa kutoka kwenye uniti 108 hadi uniti 3,000.
Tanesco inasemaje?
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) Mhandisi Felhesmi Mramba anasema Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya umeme kuhakikisha umeme mkubwa unapatikana hasa katika kipindi hiki ambapo nchi iko katika harakati za kuingia kwenye uchumi wa viwanda. “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli anataka tuongeze umeme ili nchi iwe ya viwanda na Tanesco inawajibika kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana na tumejipanga vizuri katika hilo,” anasema Muhongo.
Miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa kwa sasa ni ujenzi wa mradi wa kusambaza umeme wa Uti wa Mgongo ‘Backbone’ ambapo Tanesco inajenga mifumo ya njia kubwa za umeme wa msongo wa kilovoti 400 (Iringa- Dodoma-Singida-Shinyanga). Anasema mradi huo utagharimu trioni moja ikiwa ni fedha za serikali.
“Mradi huo utakuwa wa uti wa mgongo katika nchi kwani yakwenda kumaliza matatizo yote ya kukatika katika kwa umeme na maeneo yaliyokuwa yakipata umeme mchache hasa yale ya Mwanza na Arusha”. “Mradi huu utaboresha sana umeme matatizo yote ya umeme katika Kanda ya Ziwa na kaskazini yatakwisha,” anasema. Anabainisha kuwa ujenzi wa mradi kutoka Iringa hadi Dodoma unakamilika na kutoka Dodoma hadi Singida kazi zinaendelea ambapo kutoka Singida hadi Shinyanga mradi uko katika hatua za mwisho za kukamilika.
“Katika nchi yoyote hakuna maendeleo bila umeme na mkakati wa serikali wa kuingia kwenye uchumi wa viwanda unataka kuwe na umeme wa kutosha”. Pia mradi mwingine mkubwa wa umeme kutoka Singida hadi Nairobi unatarajiwa kujengwa na mkandarasi amepatikana. “Tutazungumza na Serikali ya Ethiopia ili tununue umeme kwao hata megawati 400 kutokana na nchi hiyo kuwa na umeme mwingi, ” anasema Muhongo.

Aidha anasema wanaendelea kuboresha miundombinu ya umeme wa gesi kwani lengo ni kufikia megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025 na kazi zinaendelea mpaka watakapoona hali ya umeme nchini imekuwa nzuri.

0 comments:

Post a Comment