NYUMBA anayoishi Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame iliopo Kijichi nje kidogo ya mji wa Unguja imeshambuliwa kwa kulipuliwa kwa bomu na kuharibika vibaya sehemu ya paa la juu pamoja na dari.
Aidha polisi visiwani hapa, kutokana na ukubwa wa matukio yanayojitokeza Unguja na Pemba yakihusisha milipuko, imeamua kuongeza nguvu na kuomba msaada kutoka kwa vikosi vingine vya ulinzi likiwemo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kukabili hujuma hizo kuelekea katika uchaguzi wa marudio.
Kamishna Makame alisema shambulio hilo lilitokea juzi saa 5 usiku na kuharibu paa la nyumba yake na kusababisha majeraha kidogo kwa baadhi ya watu waliokuwemo; ambao walipatiwa matibabu.
“‘Ni kweli nyumba yangu ninayoishi huko Kijichi iliharibiwa kwa kulipuliwa na bomu na kuharibika vibaya sehemu ya juu ya paa pamoja na dari...ilipofika saa tano tuliona moto wa mlipuko na kusikia kishindo kikubwa huku paa liking’olewa,” alisema.
Alisema uchunguzi wa awali unaonesha kwamba mlipuko uliotumiwa kuharibu nyumba yake, unafanana na uliotumika Kisonge katika maskani ya Chama Cha Mapinduzi. Hata hivyo alisema ni mapema kwa sasa kusema jambo lolote kwa sababu uchunguzi wa kisayansi unaendelea.
Awali, Makame alisema jumla ya watu 31 wanashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi Pemba wakihusishwa na matukio mbali mbali kisiwani humo ikiwemo uchomaji wa maskani za CCM na nyumba za kuishi.
Alisema matukio hayo ya uhalifu yenye lengo la kuwatisha wananchi na kujenga mazingira ya hofu, Polisi imelazimika kuongeza nguvu kwa kushirikiana na vikosi vingine ikiwemo JWTZ. Aliwataka wananchi kutokuwa na hofu wala wasiwasi wanapoona askari wa vikosi vya ulinzi mara kwa mara katika maeneo mbalimbali Unguja na Pemba.
Alisema hiyo ni sehemu ya juhudi za kupambana na matukio ya uhalifu yanayopangwa na vikundi maalumu yakilenga zaidi kisiasa na kuwafanya wananchi washindwe kujitokeza katika uchaguzi wa marudio wiki ijayo.
“Kutokana na ukubwa wa tatizo la matukio ya uhalifu yakilenga kujenga hofu na wasiwasi mkubwa kwa wananchi katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa marudio tumeamuwa kuongeza nguvu katika kuimarisha doria katika sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba...tunataka watu wapige kura kwa amani na utulivu,” alisema.
Alifahamisha kwamba wapo watu au kikundi cha watu wachache, wanalazimisha Zanzibar kuingia katika vurugu za kisiasa, amani itoweke baadaye walaumu Polisi kwamba imeshindwa kudhibiti fujo za aina hiyo. Alisema Polisi kwa mujibu wa katiba imepewa majukumu ya kusimamia amani na utulivu pamoja na kulinda mali za raia.
Alisema hawatakubali kuona kikundi cha watu wachache wanatumia fursa hiyo kuvuruga amani iliopo ambayo nchi jirani wamekuwa wakituonea choyo. “Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa watu au kikundi cha watu, waache kujishughulisha na matukio yanayohatarisha amani na utulivu wa nchi kwani amani ya nchi ikivunjika chombo cha kulaumiwa ni Jeshi la Polisi,” alisema.
Alisema ulinzi utaimarishwa katika maeneo ya mitaa ya mji wa Unguja hadi katika vituo vya kupiga kura katika siku ya uchaguzi wa marudio utakaofanyika Jumapili. Aidha, alisema utaimarishwa pia siku ya kutangazwa matokeo ya kura za urais na wawakilishi pamoja na madiwani.
0 comments:
Post a Comment