KESI inayomkabili mchezaji mkongwe wa timu ya Simba Mwinyi Kazimoto
ya shambulizi la kudhuru mwili dhidi ya mwandishi wa habari wa Kampuni
ya Mwananchi Communications Ltd, Mwanahimba Richard imeanza kusikilizwa
katika
Mahakama ya Hakimu Mfawidhi mkoa wa Shinyanga.
Akisomewa shitaka hilo mahakamani hapo na mwanasheria wa serikali,
Upendo Shemkole alisema mshtakiwa alitenda kosa la shambulizi la kudhuru
mwili Februari 10 mwaka huu, katika uwanja wa CCM Kambarage baada ya
mazoezi. Ilielezwa mahakamani hapo kuwa mchezaji huyo alionekana
kumshambulia mwandishi wa habari Mwanahimba Richard.
Hata hivyo, mshitakiwa Mwinyi Kazimoto baada ya kusomewa shitaka hilo
alikana kutenda kosa hilo, na kuiomba Mahakama kumpatia mwezi mmoja ili
atafute wakili wa utetezi wake, ombi ambalo lilikubaliwa.
Hakimu Mkazi Mfawidi wa mahakama hiyo, Rahim Mushi anayesikiliza kesi
hiyo alisema imeahirishwa hadi Machi 21 mwaka huu, ndipo itaendelea
tena kusikilizwa ili kutoa fursa kwa mshtakiwa kupeleka wakili wake wa
utetezi.
Jumla ya mashahidi sita wanatarajiwa kutoa ushahidi mahakamani hapo
katika kesi hiyo inayomkabili kiungo mchezaji wa Simba Mwinyi Kazimoto,
ambapo pia alipatiwa dhamana Sh 500,000 na Mwanasheria wa Halmashauri ya
wilaya ya Shinyanga, Batromeo Lwela.
0 comments:
Post a Comment