Tuesday, 23 February 2016

Baraza lampongeza Rais kuzuia sukari ya nje

BARAZA la Kilimo na Mifugo Tanzania (ACT), limempongeza Rais John Magufuli kwa kuagiza vyombo vinavyohusika kusitisha uingizaji wa
sukari kiholela nchini.
Kwa kuwa bado uzalishaji wa sukari nchini hautoshelezi mahitaji, baraza hilo limeshauri kuwekwa mazingira mazuri ili wawekezaji waanzishe mashamba mapya ya miwa na wakulima wadogo wawezeshwe kustawisha miwa kwa tija.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari nchini Dar es Salaam jana, baraza hilo limepongeza hatua hiyo ya Dk Magufuli ikiwemo kusisitiza kwamba kama kuna upungufu, kujazia kwake kufanyike kwa utaratibu ulio rasmi na wa wazi.
Ilisema katika kipindi cha nyuma, kutokana na uzalishaji sukari kutotosheleza mahitaji, Serikali iliamua kutoa vibali kwa wafanyabiashara kuingiza bidhaa nchini ili kufidia upungufu.
“Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu waliopewa vibali, walivitumia vibaya kwa maana ya kuagiza sukari nyingi zaidi ya mahitaji halisi. Kwa kuwa nchi zinazozalisha sukari zinatoa ruzuku kwa wazalishaji, wanao uwezo wa kupunguza bei bila kupata hasara. Hii ina maana kwamba wanaozalisha sukari nchini, kamwe hawawezi kushindana na sukari inayoagizwa kutoka nje,” ilisisitiza.

0 comments:

Post a Comment