WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewaagiza wawekezaji wenye kampuni zinazotafuta gesi na mafuta nchini kuhakikisha wanaharakisha kukamilisha miradi yao ili gesi nyingi
zaidi ichimbwe na kuongeza uzalishaji umeme.
Alisema, Serikali imedhamiria kuwa na uchumi wa viwanda ambavyo vitaendeshwa kwa rasilimali za nchini.
Alisisitiza gesi ndio injini ya kunyanyua uchumi huo kwani ndio itakayotumika kuzalisha umeme ambao utatumika katika viwanda hivyo.
“Hivyo nataka miradi yenu ya kuchimba gesi iende kwa kasi, tunataka gesi hiyo izalishe umeme mwingi, itumike kuzalishia mbolea, itumike nyumbani na pia tunataka kuiuza nje ya nchi,” alisema Profesa Muhongo.
Aliwaambia wawekezaji hao kuwa malengo ya Serikali ni kuwa nchi yenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 na njia ya kufikia huko ni kuongeza uzalishaji wa umeme.
Alisema ili kufikia lengo hilo ni lazima uzalishaji wa umeme uwe umeongezeka kutoka megawati 1,500 za sasa hivi hadi kufikia megawati 10,000.
“Tukifikia huo ukuaji wa uchumi utatoka hapa tulipo wa asilimia saba ambayo wataalamu wamekiri kuwa kiwango hicho hakiwezi kupunguza umaskini wa Mtanzania, tunataka ukuaji wa uchumi ufikie walau asilimia 10, hapo ndipo umaskini kwa watu wetu utaanza kupungua,” alisema.
Alisema viwanda vya mbolea vitajengwa viwili Kilwa na Lindi. Kuhusu kuuza nje ya nchi gesi asilia, alisema watajenga kiwanda cha kusindika gesi maeneo ya Lindi ambayo itakuwa inauzwa nje na nchi inapata fedha za kigeni.
0 comments:
Post a Comment