SEKTA Binafsi Tanzania (TPSF) imesema ina imani Serikali iliyopo madarakani na itasaidia kuleta ushindani ulio sawa katika biashara kwenye soko la ndani kutokana na jitihada inazozifanya
kuhakikisha kila mfanyabiashara analipa kodi.
Aidha, imesema hatua za Serikali kukomesha rushwa kwenye taasisi zake na kwingineko, itawawezesha wazalishaji wa ndani kupata haki kwenye soko lao, kwa kuwa usawa katika ushindani wa kibiashara utakuwepo.
Mkurugenzi Mtendaji wa sekta hiyo, Geoffrey Simbeye alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizindua maadhimisho ya Siku ya Viwango Afrika yanayoadhimishwa kitaifa nchini kwa wafanyabiashara kuonesha na kusajili bidhaa zao zishindanishwe kupata 50 zenye viwango vya ubora zaidi.
“Tunaona mkazo unaotiliwa na Serikali kuhusu wafanyabiashara kulipa kodi. Tunaishukuru na kumpongeza Rais John Magufuli kwa sababu ameonesha kuthamini wazalishaji wa ndani pia kwa kusisitiza suala la usawa wa kibiashara kwa kila mhusika kulipa kodi na umuhimu wa kuzalisha bidhaa zenye ubora,” alisema Simbeye.
Alieleza kuwa TPSF ilifanya utafiti kujua sababu za bidhaa zinazozalishwa nchini kuwa na bei ya juu kuliko zinazoagizwa kutoka nje na kubaini kuwa ni rushwa na baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kodi na ushuru.
Kwa upande wake, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambalo ni muandaaji wa sherehe za maadhimisho hayo kwa ushirikiano na TPSF limesema linawaandaa wafanyabiashara wa ndani kufaidi soko la Afrika kwa kuwa na viwango bora vya huduma na bidhaa.
Katika hotuba yake, Mkurugenzi wa shirika hilo, Joseph Masikitiko alisema uzalishaji wa bidhaa zenye viwango vilivyothibitishwa ni fursa nzuri ya kutawala soko ndani na nje ya nchi.

0 comments:
Post a Comment