YANGA itamkosa mshambuliaji wake Mzimbabwe, Donald Ngoma katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kesho dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius.
Ngoma ambaye juzi aliiongoza Yanga kushinda mabao 2-1 katika hatua ya 16 bora Kombe la FA aliondoka Dar es Salaam jana kwenda kwao Zimbabwe baada ya kufiwa na
mdogo wake, iliyeelezwa alikufa uwanjani nchini humo juzi.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema jana kuwa wamesikitishwa na kukosekana kwa Ngoma, lakini hawana jinsi na kusisitiza kuwa waliobaki wataongoza jahazi la Yanga.
“Tutamkosa Ngoma aliyeenda kwao Zimbabwe, kwenye maziko ya mdogo wake aliyefariki uwanjani Jumatano iliyopita, lakini bado tuna kikosi imara ambacho kitatuwakilisha vizuri kwa kupata ushindi mnono kama tulivyokusudia,” alisema Mwambusi bila kufafanua.
Hata hivyo Mwambusi alisisitiza Yanga ipo vizuri na ana matumaini makubwa kwamba watafunga idadi kubwa ya mabao kesho kwani wapinzani wao si timu ya kutisha.
Yanga ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0, ikiwa ugenini Uwanja wa George V, Mauritius, wiki mbili zilizopita na Jumamosi itakuwa na nafasi nzuri ya kuonesha makali yake itakapokuwa inacheza mbele ya mashabiki wake.
Akizungumzia mchezo huo, Mwambusi alisema wana uhakika wa kushinda kutokana na kuwajua vizuri wapinzani wao Cercle de Joachim, baada ya kuwaona kwenye mchezo wa kwanza.
“Tumejiandaa kucheza kwa kasi muda wote wa mchezo, tofauti na ilivyokuwa kule kwao ambapo tulikuwa hatuwajui vizuri na kulazimika tucheze kwa tahadhari, lakini mvua pia ilichangia tusioneshe kiwango chetu kilichozoeleka,” alisema Mwambusi.
0 comments:
Post a Comment