LICHA ya Chama cha Wananchi (CUF) na vyama vingine sita vya siasa
kuandika barua ya kueleza kutoshiriki Uchaguzi Mkuu wa marudio
uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha amesema
ofisi yake bado
inawatambua wagombea wa vyama hivyo.
“Mgombea Urais wa CUF na wagombea wake wa Baraza la Wawakilishi na
Madiwani, na vyama vingine sita waliandika barua kwa ZEC wakisema
hawatashiriki uchaguzi huo. Kwa bahati mbaya, wagombea wote na vyama
vyao vya siasa vinavyodai kususia, wameshindwa kufuata taratibu.
“Inaelezwa wazi katika Kifungu cha 31 na 37A na Sura ya 46 na 50 ya
Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, kuhusu taratibu za uteuzi wa wagombea na
jinsi gani wagombea wanaweza kujitoa katika uchaguzi. Hakuna hata
mgombea mmoja aliyefuata sheria hiyo,” alisema Jecha katika taarifa yake
kwa vyombo vya habari jana.
Jecha alisema kulingana na kanuni, ni jukumu la chama cha siasa
kuandika kwa ZEC kuhusu kuondoa udhamini wake kwa mgombea. Alisema hata
CUF ambayo mgombea wake ni Maalim Seif Shariff Hamad, imeshindwa kufuata
kanuni hizo.
“Ni muhimu sana kuelewa na kufuata sheria za uchaguzi. Tumekuwa
tukiwasiliana na vyama vyote 14 vya siasa, sambamba na kusambaza vifaa
vya uchaguzi kwa wilaya zote kumi na moja kabla ya kuvitawanya baadaye
kwenye vituo 1,580 vya kupigia kura,” alisema Jecha.
Alisema wagombea wote 14 wa urais, watu wanaowania Uwakilishi kutoka
katika majimbo 54 na wagombea 111 katika ngazi ya Udiwani, bado
wanaendelea kutambulika kama wagombea halali kwa uchaguzi wa mwezi ujao.
Jecha amekiri kupokea barua kutoka CUF na vyama vingine sita wakisema
hawatashiriki uchaguzi huo, wakati vyama vingine vinane kikiwamo CCM,
ACT, ADC CCK AFP, SAU, TLP na ADA-TADEA vimethibitisha kushiriki.
“Tunakamilisha taratibu ili kuwapatia wagombea wote wa urais ulinzi
kwa saa 24 hadi wakati matokeo ya uchaguzi yatakapokuwa yametangazwa,”
alisema Jecha na kuongeza kuwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
litawekwa katika sehemu mbalimbali ili wapiga kura waone vituo vyao vya
kupigia kura.
Alisema kuwa maandalizi kwa ajili ya marudio ya uchaguzi huo
yanaendelea vizuri na tayari uteuzi na kuajiri maofisa wa uchaguzi na
wafanyakazi wengine umefanyika na kufuatiwa na mafunzo kuhusu jinsi gani
ya kusimamia vizuri uchaguzi.
Alisema mafunzo kwa ajili ya wasimamizi wa uchaguzi (ngazi ya
majimbo) yanatarajiwa kuanza leo hadi Februari 28, wakati mafunzo kwa
maofisa wa vituo vya kupigia kura yataanza Machi 11 hadi 13, mwaka huu.
Mafunzo kwa ajili ya mawakala wa vyama vya siasa na maofisa wa
kusimamia usalama yatafanyika Machi 14 na 15, mwaka huu, kwa mujibu wa
Mwenyekiti huyo wa ZEC.
Mwenyekiti huyo wa ZEC alisema maandalizi ya awali ya kuchapisha
karatasi za kura yamekamilika, na mchapaji ambaye hakutaka kumtaja
anaendelea na kazi ya kuchapa karatasi hizo ambazo zinatarajiwa kuletwa
Zanzibar mapema mwezi ujao.
“Tunawaomba wananchi wajiandae kwa uchaguzi wa marudio na wagombea
wote kutoka vyama tofauti vya siasa kufuata kanuni na sheria za
uchaguzi,” alisema Jecha.
Uchaguzi huo wa marudio wa Machi 20, mwaka huu utafanyika baada ya
ule wa Oktoba 25, mwaka jana, kufutwa kutokana na kasoro mbalimbali
zilizoufanya usiwe huru na wa haki. Juhudi za kuwapata wasemaji wa CUF
jana hadi tunaenda mitamboni hazikufanikiwa.
0 comments:
Post a Comment