RAIS
John Magufuli amesema hatua anazochukua dhidi ya watumishi wa umma
waliofanya ubadhirifu serikalini na taasisi zake zinalenga kuwarudisha
kwenye maadili ya utumishi wa umma, kufuata misingi ya kazi na sio
vinginevyo.
Alisema
hayo jana katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Burka mjini hapa
alikoshiriki ibada na waumini wa kanisa hilo. Rais Magufuli alisema
watumishi wa umma walijisahau, wakafanya ubadhirifu na kukiuka kwa
makusudi maadili ya kazi kwa hali ya juu na kufanya Watanzania wanyonge
kuendelea kuteseka wakati wao wakiendelea kuishi maisha ya peponi.
Alisema
anapambana na watumishi hao kwa hali na mali na atawasimamisha kazi na
hata kuwafukuza kazi kwa kuwa aliahidi kutetea wanyonge. Alisisitiza
hilo kwake halitarudi nyuma. Rais alisema yeye sio mkatili wala jeuri
kama ambavyo baadhi ya watu wanafikiria.
Alisema
kwa hali ilivyokuwa, ni lazima achukue hatua madhubuti kwa watumishi wa
umma walioifilisi nchi kwa manufaa yao, iweze kusonga mbele. ‘’Mimi sio
mkatili wala jeuri, lakini ni lazima uchukue hatua kwa watumishi wa
umma walioifikisha nchi hapa tulipo,’’ alisema.
Aliongeza
kusema; “Nimejitoa kafara kwa ajili ya wanyonge kama nilivyoahidi
kipindi nilipokuwa naomba kura kutaka niwe Rais na hilo litawaudhi
baadhi ya watu wakubwa, lakini itabidi wanivumilie tu.
“Niko
pamoja na ninyi ndugu zangu Watanzania na wana Arusha wote, napenda
kuwaahidi tena sitawaangusha, nitasimama mbele kuwatetea masikini. Siku
zote nitakuwa upande wenu, siku zote nitatembea na ninyi, nasema kwa
dhati kabisa na nataka muamini hilo kwamba sitawaangusha,” alisema
Magufuli huku akishangiliwa na waumini walioshiriki ibada hiyo.
Rais
ambaye alisisitiza kukerwa na hali mbaya ya kimaisha ya Watanzania
wanyonge wakati baadhi ya watumishi wa umma wakiishi kama wako peponi,
alisema kasi yake ya kupambana na watumishi hao hataipungua kamwe na
ndiyo kwanza inaanza.
“Najua
baadhi ya wakubwa watakerwa na hatua ninazochukua, kwa hiyo nawaomba
Watanzania mniombee kwa Mungu ili niweze kufanya kazi yangu kwa amani
kubwa, ‘’Watumishi wamejisahau na wamekuwa wakifanya kazi kinyume na
maadili ya utumishi wa umma na hatua ninazochukua msizitafsiri kuwa ni
ukatilii au udikteta hapana,’’ alisema.
Rais
Magufuli alisema, ‘’Watumishi wa umma wamekuwa wakiwadhulumu Watanzania
kwa muda mrefu kwa kuwanyonya jasho lao; hivyo ni lazima maamuzi ya
kuwarudisha katika mstari yachukuliwe.”
Alisema
ili nchi iweze kupiga hatua lazima kuwe na nidhamu ya kazi, uadilifu na
kuwajibishana linapokutwa kosa. Alisema bila ya hivyo, nchi haiwezi
kusonga mbele itakuwa ni kujidanganya. Rais aliongeza kuwa Watanzania
wanyonge ni lazima wapate haki yao pale wanapohitaji na kutokuwa na
matabaka ya walionacho na wasio nacho.
“Ninajua
kuongoza ni kazi kubwa, ninajua kuongoza taifa lililo masikini kama
Tanzania inahitaji mkono wa Mungu, kwa hiyo niwaombe sana ndugu zangu
Wakristo na Watanzania kwa ujumla, muendelee kuliombea taifa hili,
kuniombea mimi, na pia kujiombea sisi wote ili amani tuliyonayo katika
nchi yetu iendelee kudumu katika maisha yote.
“Lakini
siku zote katika matendo yetu kila tunapofanya tumtangulize Mungu kwa
sababu Mungu ndio kila kitu, lakini tutambue kwamba siku moja tutakufa,
kwa hiyo ni vyema katika matendo yetu tutakapokuwa hapa duniani
tujitahidi sana kufanya matendo mazuri kwa ajili ya watu na hasa watu
wanyonge, ambao kwa kweli Watanzania waliowanyonge wanapata shida sana,”
alisema.
Akihubiri
kwenye ibada ya misa takatifu kanisani hapo, Padri Geramani Longoi,
aliwataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii na kuwa waadilifu kazini.
Katika misa hiyo ya Siku Kuu ya Kupaa Mbinguni kwa Yesu Kristo, Longoi
alisema hata Yesu Kristo alifanya kazi yake duniani na baada ya
kuwatumikia ipasavyo wanadamu, alipaa mbinguni.
Mwenyekiti
wa Parokia hiyo, Jonathan Mushi aliwataka Watanzania kumuunga mkono
Rais Magufuli kwa kazi ngumu anayofanya. Mushi alisema kila Mtanzania
mwenye nia njema na nchi yake, hanabudi kumuunga mkono Rais Magufuli kwa
kuwa uamuzi anaouchukua ni mgumu. Alisema uamuzi wake unataka kila
mmoja kufuata maadili ya kazi na kuwa muadilifu.
0 comments:
Post a Comment