Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza rasmi
kutoitambua Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), inayoongozwa na Dk Ali
Mohamed Shein.
Mbali na kutoitambua Serikali hiyo, chama hicho kimesema leo kitatoa
mkakati mzito wa namna ya kushughulikia suala la matangazo ya Bunge la
Kumi na Moja kutoonyeshwa moja kwa moja (live) na televisheni.
Msimamo huo ulitangazwa kwa waandishi wa habari jana mjini Dodoma katika
kikao cha pamoja kati ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji,
manaibu wake wawili, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).
Pia walitoa taarifa juu ya mambo yanayojadiliwa katika kikao cha siku
mbili cha Kamati Kuu (CC) kinachofanyika chini ya Mwenyekiti wake,
Freeman Mbowe.
Akizungumzia hali ya kisiasa Zanzibar, Mwalimu alisema chama hicho hakitampa ushirikiano Dk Shein.
“Kikao maalumu cha Kamati Kuu ya Chadema kilichoketi Jumatatu, tumefikia
msimamo wa kutoitambua Serikali ya SMZ. Msimamo wa Maalim Seif Shariff
Hamad ndiyo msimamo wetu,” alisema.
Maalim Seif aliwania urais Zanzibar kupitia CUF katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 25, mwaka jana kabla ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kufuta
matokeo yake na kutangaza uchaguzi wa marudio ambao mgombea huyo na
chama chake walisusia.
“Hatutatoa ushirikiano kwa SMZ na katika kikao cha leo (jana) cha CC
tutawasilisha azimio hilo.Hali ya kisiasa Zanzibar ni mbaya mbaya sana.
Wazanzibari wanaelekea kununa,” alisema Mwalimu.
Mwalimu alisema hawatafanya maandamano Zanzibar lakini hali itakuwa
mbaya zaidi kwani Wazanzibari wengi wanaelekea kununa na kwamba hilo
litasababisha hali mbaya zaidi.
“Hali ya Zanzibar si nzuri kama CCM wanavyoeleza. Watu hawazikani,
hawatembeleani tumerudi kulekule kama mwaka 1995 kabla ya kuundwa kwa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema.
Mashinji alisema kikao hicho cha kamati kuu kitapokea taarifa kutoka kwa
wabunge wa Chadema, kuhusu Bunge kutoonyeshwa ‘live’ na athari zake kwa
wananchi.
“Uhuru wa wananchi kupata habari litajadiliwa kwa kina. Sasa hivi Bunge
letu liko gizani tunapata habari za kupapasa tu. Tutatoka na mkakati
kabambe wa kushughulikia suala hili,” alisema.
Akizungumza hatua hiyo iliyochukuliwa na Bunge, Mnyika alisema
kinachoonekana sasa ni kama chombo hicho kimetekwa na Serikali na hilo
litatolewa tamko zito rasmi leo na Mbowe mwenyewe.
“Kuna mambo makubwa tuki- yawekea mkakati huwa Serikali inasalimu amri.
Tunataka kutoka kwenye huu mkwamo ili Bunge lionyeshwe live,”alisema.
Januari 27, Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
alitangaza Serikali kusitisha matangazo hayo ya moja kwa moja kama njia
ya kubana matumizi.
Waziri huyo aliliambia Bunge matangazo hayo yatarushwa vipande muhimu
vya mijadala usiku katika kipindi maalumu cha Leo katika Bunge ambacho
kitarushwa saa nne za usiku uamuzi ambao ulipingwa vikali ndani na nje
ya Bunge.
Leo, Nape atawasilisha bajeti ya wizara yake bungeni ambako mjadala
mzito unaotarajiwa kulitikisa Bunge ni suala hilo la kutoonyeshwa moja
kwa moja kwenye televisheni.
Wadau wa habari wamepiga kambi mjini hapa kujaribu kuishawishi Serikali na Bunge kubadili msimamo huo
0 comments:
Post a Comment