
MWENYEKITI wa CCM na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amekutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Dk Mario Giro kujadili mgogoro wa Libya. Dk Giro alimtembelea Kikwete ofisini kwake katika Ofisi ndogo za Makao Makuu ya CCM zilizopo mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam.
Kikwete alisema ujio wa Dk Giro unatokana na kutaka kujua hatua zilizofikiwa katika kusuluhisha mgogoro wa Libya kwani umekuwa na athari nchini mwake kutokana na nchi hizo kuwa jirani.
Kauli hiyo ilitolewa na msaidizi wa Kikwete, Seleman Mwenda wakati akitoa taarifa ya ujio wa Naibu Waziri huyo kwa waandishi wa habari. Mwenda alisema, pamoja na kuzungumzia mgogoro huo pia Dk Giro alikuja kutokana na uhusiano wa kirafiki uliopo baina yake na Kikwete kutokana na kufanya kazi pamoja kwa muda mrefu wakiwa mabalozi wa amani na kusuluhisha migogoro katika nchi mbalimbali.
“Italia ni nchi jirani ya Libya kwa hiyo kile kinachoendelea Libya kinawaathiri watu wa Italia kutokana na ujirani wao walionao. Dk Giro alitaka maelezo kuhusu Kikwete na timu yake waliyoyachukua hadi sasa,” alisema Mwenda.
Kwa mujibu wa Mwenda, Kikwete ni mmoja kati ya watu walioko kwenye timu ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa Libya, hivyo ujio huo ni wa kutaka kujua hatua zilizofikiwa kuhusu kurejesha amani Libya.
Kikwete aliteuliwa Februari Mosi, mwaka huu kuwa mwakilishi wa Umoja wa Afrika (AU) katika mchakato wa kutafuta suluhu ya mgogoro wa Libya na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja huo, Dk Nkosazana Dlamini Zuma.
Uteuzi wake ulitangazwa rasmi na AU katika kikao cha wakuu wa Nchi za Afrika kilichofanyika Addis Ababa, nchini Ethiopia mwaka huu. Tangu kuteuliwa kwake, Kikwete ameshashiriki Mkutano wa Kamati ya Uandishi ya Baraza Maalumu la Uandishi wa Katiba ya Libya ambao ulifanyika mjini Salalah, nchini Oman mwezi Machi.
0 comments:
Post a Comment