Wednesday, 24 February 2016

Yanga yahamia jeshini

BAADA ya Jumamosi kuifunga Simba mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga leo itashuka Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kumenyana na JKT Mlale ya Songea katika
mchezo wa raundi ya nne ya michuano ya Kombe la FA.
Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm aliliambia gazeti hili jana kuwa anatarajiwa kupata upinzani mkali licha ya kwamba wanacheza na timu ya daraja la kwanza.
JKT Mlale inamilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Alisema pamoja na hayo, amekiandaa kikosi chake vizuri na ana imani watapata ushindi kwenye mechi hiyo.
“Najua upinzani utakuwa mkali kesho (leo) maana tunacheza na timu ndogo kwa hiyo itataka kushinda mbele yetu,” alisema.
Yanga inaingia uwanjani kwenye mechi hiyo baada ya kutoka kumfunga mtani wake wa jadi, Simba mabao 2-0 mwishoni mwa wiki iliyopita na sasa inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi moja baada ya kufikisha pointi 46.
“Nataka tushinde kila mechi kwa sababu mashindano yote tunayoshiriki yana umuhimu mkubwa, hivyo ni vizuri kushinda,” alisema.
Kwa mujibu wa kanuni, mshindi wa Kombe la FA ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mwakani, hali inayoleta upinzani mkubwa kwani sasa mshindi wa pili wa Ligi Kuu hatashiriki michuano ya kimataifa.
Awali, mshindi wa pili alishiriki Kombe la Shirikisho michuano ambayo Azam inashiriki msimu huu baada ya kushika nafasi ya pili msimu uliopita na Yanga inashiriki Ligi ya Mabingwa baada ya kutwaa ubingwa.
Mechi hiyo pia itakuwa maandalizi tosha kwa Yanga ambayo Jumamosi itakuwa mwenyeji wa Cercle de Joachim ya Mauritius katika mechi ya pili ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga ilishinda bao 1-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Mauritius wiki mbili zilizopita na hivyo kufanya kazi ya kusonga mbele kuwa rahisi endapo itashinda ama kutoka sare Jumamosi.

0 comments:

Post a Comment