Saturday, 27 February 2016

Nape aongoza maziko ya Mapili Dar, Magufuli amlilia

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akiweka udongo katika kaburi la msanii wa muziki marehemu Kassim Mapili aliyezikwa katika makaburi ya Kisutu Dar es Salaam jana. (Picha na Yusuf Badi).
MAMIA ya wapenzi wa muziki wa dansi, wakiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnaue jana walishiriki katika maziko ya mwanamuziki mahiri nchini Kassim Mapili aliyezikwa makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.
Waombolezaji hao wakiwemo wanamuziki wenzake na wadau mbalimbali wa muziki walizungumzia kifo cha Mapili kwa nyakati tofauti na kueleza kuwa ni pigo kwa medani ya muziki w
a dansi nchini.
Katibu wa Chama cha Muziki wa Dansi nchini (Chamudata), Hassan Msumari, alisema kifo cha Mapili ambaye ni miongoni mwa waasisi wa chama hicho ni pigo kwa muziki nchini.
Kwa mujibu wa Msumari, Mapili aligundulika amekufa usiku wa kuamkia jana chumbani kwake Tabata, Dar es Salaam, baada ya majirani kuamua kuvunja mlango kutokana na kutomuona tangu Jumanne usiku alipoonekana kwa mara ya mwisho akienda kutazama mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Arsenal na Barcelona.
Wakati huo huo, Rais John Magufuli ametuma salamu za pole kwa familia ya Mapili, ambapo ameeleza kushtushwa na taarifa za kifo hicho na kuwaombea familia, wanamuziki wenzake, ndugu, jamaa na marafiki ustahamilivu na uvumilivu katika kipindi hicho kigumu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa katika salamu hizo za Rais kupitia kwa Nnauye, amemuelezea Mapili kama mwanamuziki hodari, mbunifu na aliyependwa na wapenzi wa muziki wa ndani na nje ya Tanzania na kwamba ametoa mchango mkubwa katika kuendeleza muziki huo.
“Ni vigumu kuzungumzia maendeleo ya muziki wa dansi hapa nchini pasipo kutambua mchango mkubwa wa Kassim Said Mapili na wenzake waliofanya kazi kubwa katika miaka ya sabini,” alisema Rais katika salamu hizo.
Alisema Taifa litakumbuka na kuuenzi mchango wake, sio tu kwa kuimba na kupiga vyombo bali pia kuwaunganisha wanamuziki, kuanzisha bendi za muziki wa dansi na kufanya kazi kwa umakini mkubwa. Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza amesema baraza limepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa kifo cha Mapili.
“Kassim Mapili ni msanii na mdau wa muda mrefu wa sekta ya sanaa nchini. Amekuwa ni taa na nuru ambayo katika kipindi chote cha uhai wake imeangaza na kutoa mwanga angavu kwenye sekta ya sanaa."
Alisema Mapili licha ya kuwa mwimbaji na mpigaji gitaa katika bendi mbalimbali zikiwemo za Kilwa Jazz, Polisi Jazz, Vijana Jazz na miongoni mwa wasanii waliokutana mwaka 1982 kuanzisha Chamudata.

0 comments:

Post a Comment