Thursday, 25 February 2016

HELSB yataka vyuo kuimarisha ofisi za mikopo

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imevitaka vyuo vikuu nchini kuhakikisha vinaimarisha ofisi za ofisa mikopo katika vyuo vyao ili kuwaondolea wanafunzi tatizo la kufuatilia majibu ya matatizo yao kwa Bodi.
Akizungumza jana, Meneja Habari, Elimu na Mawasiliano wa
HESLB, Omega Ngole alisema kuimarishwa kwa ofisi hizo kutaondoa usumbufu kwa wanafunzi kufuatilia matatizo yanayotokana na mikopo.
“Ni vema wadau wetu ambao ni vyuo na wanafunzi wanufaika wa mikopo yetu kutumia ipasavyo mfumo huu wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wanafunzi kuhusu mikopo. Wanafunzi wana wajibu mmoja tu wa kuhakikisha wanasoma masomo yao na si kupoteza muda kuzunguka kufuatilia matatizo hayo."
Alisema mfumo huo ambao umeanzishwa mwaka 2011, ulilenga kumfanya mwanafunzi atumie muda wake kwa ajili ya masomo na si kuhangaikia mikopo.
Alisema wanafunzi wanapopeleka malalamiko yao kwenye dawati la malalamiko katika chuo yanatakiwa kushughulikiwa ndani ya siku mbili na kama tatizo hilo ni kubwa linakwenda kwa Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma.
Ngole alisema kwa wanafunzi ambao vyuo vyao viko nje ya ofisi za kanda, wanatakiwa kuwasiliana moja kwa moja na Bodi makao makuu ambao huchukua siku mbili kushughulikia.

0 comments:

Post a Comment