Maofisa wa Polisi wamemhoji Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface
Jacob kabla ya hajakutana na waandishi wa habari kwa madai kuwa wamepata
taarifa mkutano wake huo ulilenga kumkashifu Rais John Magufuli.
Maofisa hao waliovalia kiraia walionana na Jacob ofisini kwake na
walimruhusu kuendelea na mkutano huo baada ya meya huyo kuwahakikishia
kwamba hana nia hiyo bali alitaka kutoa ufafanuzi wa baadhi ya masuala
baada ya ujio wa Rais, Kinondoni Jumanne iliyopita.
“Kwa mara ya kwanza meya anahojiwa, lakini niliwaambia wana usalama
lengo langu ni nini na sipo kwa ajili ya kumkashifu Rais, ila nafahamu
vita iliyopo kati yetu na baadhi ya viongozi,” alisema Jacob.
Pamoja na ufafanuzi huo, Jacob aliwataka baadhi yao (askari) kushiriki
kwenye mkutano huo wa wanahabari kufuatilia alichotaka kuwaeleza
wanahabari na polisi mmoja alibaki kusikiliza bila kutambulishwa.
Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Suzan Kaganda alisema hakukuwa na tatizo
lolote polisi kuwapo eneo hilo, kwani wanafanya shughuli zao za ulinzi
na usalama wa raia na hasa ikizingatiwa kuwa kuna Ofisi ya Mkuu wa
Wilaya.
Katika mkutano huo, meya Jacob alitoa ufafanuzi wa yaliyojiri Jumanne
iliyopita wakati Rais Magufuli alipofanya ziara katika manispaa hiyo na
kubatilisha umiliki wa eneo la Magomeni Kota lililokuwa mali ya
halmashauri kuwa ya Serikali Kuu.
Meya Jacob aliwaambia wanahabari kuwa uamuzi wa Serikali kuchukua eneo
hilo umeisababishia halmashauri yake hasara ya zaidi Sh4.5 bilioni
kutokana na gharama walizoingia.
Katika eneo hilo, nyumba 644 zilivunjwa mwaka 2011 kwa miadi ya kwamba
zikijengwa upya, wananchi waliokuwa wakiishi hapo wakiwa wapangaji
wangerejeshwa, lakini mradi huo ulichelewa kuanza.
Akiwa ameambatana na baadhi ya madiwani, Jacob alisema hasara hiyo
imetokana na halmashauri kutumia Sh2 bilioni kumlipa mkandarasi kwa
ajili ya michoro ya eneo litakavyokuwa.
Alisema pia manispaa hiyo imetoa Sh1 bilioni kwa mkandarasi Gulf kwa
ajili ya kuchora ramani ya ofisi mpya za halmashauri na kusimamia ujenzi
wa mradi huo na kutumia Sh700 milioni kuwalipia kodi wapangaji hao
baada ya kuwahamisha.
“Faida tuliyoipata ni kwamba wananchi tuliopanga kuwahudumia tayari Rais
amewahudumia. Hatupingi maamuzi ya Serikali, lakini wananchi watambue
kwamba manispaa haina chochote itakachokipata, bali kila kitu kitakuwa
kinafanywa na Serikali Kuu,” alisema Jacob.
Meya alisisitiza kuwa madiwani wa Ukawa hawapingi uamuzi huo ila baadhi
ya viongozi wanaomzunguka Rais hawamwambii ukweli wa mambo kuhusu mradi
wa Magomeni Kota na kwamba baadhi ya watumishi wa Serikali ndiyo
waliosababisha kufikia hatua hiyo.
“Siku ile ningepata nafasi hata dakika tatu, ningemweleza Rais Magufuli
ukweli wa mambo wa mradi huu. Lakini kuna baadhi ya viongozi
waliomzunguka waliamua kuninyima nafasi hiyo. "
Hata hivyo, Jacob alimwomba Rais Magufuli kukutana naye ili amweleze kwa
undani jambo linalomuumiza kuhusiana na masuala ya ardhi yanayoikumbuka
Kinondoni.
Alifafanua kwamba, Serikali iliyopita na manispaa hiyo ilishaingia
mkataba na kampuni ya Blue Marine ya Romania kwa ajili ya ujenzi wa
mradi wa Magomeni Kota ambao ulifikia katika hatua nzuri lakini baadhi
ya watumishi wa Serikali waliamua kuweka ‘kauzibe’ na kuipa sifa mbaya
Kinondoni.
“Tulikuwa tunasubiri utiaji wa saini kutoka Serikali Kuu, lakini baada
ya kuona Kinondoni inaongozwa na Ukawa wameamua kuleta ‘figisufigisu’ za
kuukwamisha,” alisema Jacob.
Katika ziara hiyo, Rais Magufuli alielezea kusikitishwa kwake na namna
tatizo la wakazi hao lilivyoshughulikiwa na kuwaahidi kuwa Serikali yake
itahakikisha hawasumbuliwi.
0 comments:
Post a Comment