Tuesday, 10 May 2016

Watumishi hewa 38 zaidi wanaswa Dar

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
ONGEZEKO la watumishi hewa bado limeendelea kuutesa mkoa wa Dar es Salaam, kwani katika siku saba za ufuatiliaji wamebainika watumishi hewa wengine 38 walioitia hasara serikali ya Sh milioni 724.
Wamepatikana baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda kuwasainisha mkataba wakuu wote wa idara na kutoa siku saba kuhakikisha wanahakiki watumishi waliopo ili kuwaondoa watumishi hewa.
Manispaa ya Ilala imekutwa na watumishi 11 wasiojulikana ambao walikuwa wakilipwa mishahara tangu mwaka 2010, hali iliyomlazimu Makonda kumsimamisha kazi Ofisa Utumishi wa Manispaa hiyo, Francis Kilawale kwa kushindwa kuwatambua watumishi hao na kukubali kuwalipa mishahara.
Ongezeko hilo limefanya mkoa wa Dar es Salaam kuwa na jumla ya watumishi hewa 248 ambao wametia hasara serikali ya Sh bilioni 3.6 baada ya kulipwa mishahara.
Akiorodhesha watumishi hao katika Manispaa zote za Jiji, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando alisema Manispaa ya Temeke imekutwa na watumishi hewa 21 walioigharimu serikali zaidi ya Sh milioni 222, Ilala watumishi 39 ambao wamesababisha hasara ya Sh milioni 382 huku Manispaa ya Kinondoni ikiwa na watumishi hewa 14 walioigharimu serikali kiasi cha Sh milioni 120.
Akizungumzia suala hilo wakati wa mkutano na Wakuu wa Idara wa Jiji jana, Makonda alisema ni jambo la kushangaza kuona kuna watumishi wasiojulikana na wanalipwa mishahara, kwani inaonesha wakuu wa idara hawafanyi kazi zao kama inavyotakiwa.
Aidha, amewataka wakurugenzi wa manispaa zote kuwachukulia hatua wakuu wa idara ambao wameshindwa kufanya kazi zao kwa ufasaha ili kuondoa malalamiko katika idara hizo. Ametoa wiki mbili kwa wakurugenzi hao kuhakikisha wanamaliza suala la watumishi hewa. Amewataka pia kueleza hatua zilizochukuliwa kwa waliobainika ni watumishi hewa.

0 comments:

Post a Comment