Friday, 1 April 2016

Pluijm awaingiza chaka Al Ahly

PluijmKocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm.
Wilbert Molandi, Dar es Salaam
YANGA ina taarifa kuwa wapinzani wao Al Ahly wamepata video za mechi zao, lakini Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm amesema atawavaa wapinzani wao hao kwa staili nyingine kabisa.
Yanga inatarajiwa kuvaana na Al Ahly, Aprili 9, mwaka huu katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar kisha kurudiana Aprili 19, 2016 nchini Misri.
Timu hiyo, itavaana na Al Ahly katika mchezo wa hatua ya tatu ya mtoano wa michuano hiyo baada ya kuwatoa Cercle de Joachim ya Mauritius na baadaye APR ya Rwanda.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Pluijm alisema kila siku anabuni mbinu na staili mpya ambazo anaamini zitawaondoa Waarabu hao kwenye hatua hiyo ya pili ya michuano hiyo.
Pluijm alisema wakati yeye akipanga mikakati hiyo kuwaondoa, nao wapinzani wake wanaweka mipango mingi ya kuwatoa katika michuano hiyo, hivyo anaamini mechi zote mbili zitakuwa ngumu kwa pande zote.
“Lazima tujiandae vya kutosha kabla ya kukutana na Al Ahly, kwani hautakuwa mchezo mwepesi kwetu wala kwao, lakini sina budi kukitazama kikosi changu kwa hali zote, ninahitaji kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
“Kwani ni lazima tuanze vema kwenye uwanja wetu wa nyumbani kabla kuelekea kwao huko Misri kwenda kurudiana tukiwa tuna ushindi mkubwa ili tujitengenezee mazingira mazuri.
“Ninachokifanya ni kuwaongezea mazoezi wachezaji wangu katika mazoezi yangu ya kila siku kwa kubuni staili na mbinu mbadala zitakazotupa ushindi kwa kuanzia mechi hii ya kwanza tutakayoicheza nyumbani,” alisema Pluijm.

0 comments:

Post a Comment