Thursday, 7 April 2016

Kijazi: Hatufurahii kutumbua majipu


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi.

KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, amesema hatua za kutambua majipu kwa baadhi ya viongozi wasio waadilifu inayochukuliwa na serikali ya awamu ya tano, siyo kwamba wanafurahia bali wanalazimika kufanya hivyo kurejesha maadili katika utumishi wa umma ambayo yalikuwa yameanza kupotea.
Amesema kwa kipindi kirefu kidogo, maadili hayo yalionekana kupotea kwa watumishi wengi wa umma ikiwamo baadhi yao kuendekeza rushwa pale wananchi wanapotaka huduma kutoka kwao.
Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akifungua mafunzo ya maadili kwa watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma.
Balozi Kijazi alisema mmomonyoko huo wa wa maadili ni changamoto kubwa ambayo kwa namna moja umechangia hata kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma.
Balozi Kijazi alisema kama ndani ya serikali, hakuna maadili ni vigumu hata kwa wananchi kuwa na imani nayo. 
"Hatutasita kumchukulia hatua kiongozi yeyote wa umma atakeyebainika kukiuka taratibu za utumishi wa umma, alisisitiza.
Kwa upande wake, Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu Salome Kaganda, alisema changamoto inayoikabili Sekretarieti ya Maadili ni kuwapo kwa sheria ya maadili ambayo haitoi mamlaka na nguvu za kuifanya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Kuhusu taarifa za mali za viongozi hao, alisema hadi sasa utekelezaji wake ni mzuri.

0 comments:

Post a Comment