Monday, 7 March 2016

Utouh aanzisha taasisi kuhimiza utawala bora

ALIYEKUWA Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh
ALIYEKUWA Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, amesema uwepo wa taasisi zisizo za kiserikali zinazohusu uwajibikaji na utawala
bora kunachangia utekelezaji wa dhana ya uwajibikaji na utawala bora nchini.

Utouh aliyasema hayo jana, Dar es Salaam wakati akitambulisha Taasisi ya Fikra ya Uwajibikaji Tanzania aliyoianzisha kwa kushirikiana na aliyekuwa Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Yonna Killagane.
Utouh ambaye ndiye Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo alisema, imeanzishwa kwa lengo la kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya uwajibikaji na utawala bora katika usimamizi wa rasilimali za umma.
Alisema uanzishwaji wa taasisi hiyo utajenga uhamasishaji wa wananchi kwenye ushiriki katika masuala ya uwajibikaji na utawala bora ambao ni jambo la msingi kuhakikisha maendeleo yanapatikana.
“Kama jitihada za kuimarisha uwajibikaji nchini zitaachiwa Bunge na taasisi za usimamizi za serikali pekee yao, uwezekano wa kufanikisha utekelezaji huu utakuwa mdogo kwa sababu suala la uwajibikaji linahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali ili kuleta tija kwa taifa,” alisema Utouh.
Alisema kuwa taasisi hiyo pia itajikita katika kuchambua mifumo iliyopo na kufanya utafiti wa masuala ya uwajibikaji ili kuendeleza jitihada na mafanikio yaliyopatikana nchini ambayo ni muhimu kwa ukuzaji wa dhana ya uwajibikaji na utawala bora.
Akizungumzia malengo mengine ya taasisi hiyo, Utouh alisema, taasisi hiyo inakusudia kupitia na kuchambua taarifa zilizotolewa na taasisi za usimamizi nchini kwa madhumuni ya kutoa mapendekezo ya kuelimisha wananchi na kuisaidia serikali kuchukua hatua stahiki.
Pia alisema itafanya taarifa na ripoti za taasisi za usimamizi kuwa rahisi na rafiki zaidi kusomeka na kutumika kwa wananchi walio wengi, ambao angalau wanajua kusoma na kuandika na kuwa na fursa za kuhusisha wadau kwenye midahalo ya uwajibikaji.
Aidha alisema ili kufikia malengo taasisi hiyo imeandaa mkutano wake wa kwanza wa kimataifa utakaohusu uwajibikaji katika sekta ya gesi asilia na mafuta kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hiyo kwenye maendeleo ya nchi.
“Huu utakuwa ni mkutano muhimu sana na sahihi kwa watu wote wanaojihusisha na masuala ya uwajibikaji na utawala bora katika mafuta na gesi hususan wahasibu, wanasheria, wahandisi na wote walio katika nyadhifa za usimamizi,” alisisitiza.
Alisema mkutano huo unatarajiwa kufanyika Aprili 11 na 12 jijini Dar es Salaam na unatarajiwa kuwashirikisha wazungumzaji mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi. Kwa mujibu wa Otouh, Tanzania katika mkutano huo itakuwa na washiriki 100 na kutoka nje ya nchi wanatarajiwa kufika wageni 50.

0 comments:

Post a Comment