MAWAZIRI wa Serikali ya Awamu ya Tano wamewajia juu wabunge wa upinzani
na wananchi wanaovishutumu kila mara vyombo vya ulinzi nchini na
kuwataka kuacha kuvihusisha vyombo hivyo na masuala ya kisiasa.
Mawaziri hao ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein
Mwinyi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January
Makamba.
Wamewataka wananchi na hususani wabunge wa vyama vya upinzani, kutambua
kuwa vyombo hivyo vya ulinzi ambavyo ni pamoja na Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Polisi wajibu wake mkubwa ni kulinda
mipaka ya nchi na usalama wa raia na mali zao.
Akizungumza wakati wa mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na
matumizi ya Wizara inayoshughulikia Muungano na Mazingira, Dk Mwinyi
alisema haijawahi kutokea na wala haitotokea jeshi kutumika kisiasa.
Alisema Jeshi la Tanzania limekuwa likitekeleza majukumu yake kwa
kufuata sheria iliyojiwekea pamoja na za kimataifa na wala hata siku
moja haliwezi kutumika kwa ajili ya kutumiza malengo ya kundi fulani.
“Jeshi letu lina sifa ya kimataifa ya ulinzi wa amani, dunia kote
tunasifika kwa weledi, kulinda amani na mipaka yetu. Haijawahi kutokea
wala haitotokea jeshi kujiingiza kwenye shughuli za kisiasa,”
alisisitiza Dk Mwinyi.
Alisema tangu mjadala wa makadirio ya bajeti hiyo uanze, baadhi ya
wabunge hususani wabunge wa upinzani wamekuwa wakilitupia shutuma nzito
jeshi na vyombo vya dola kwa ujumla kuwa limetumika vibaya kwenye
uchaguzi wa Zanzibar na chaguzi nyingine.
Aliwataka wabunge hao pamoja na wananchi wanaovilaumu mara kwa mara
vyombo hivyo vya dola kumuogopa Mungu kwa kutoa madai ya uongo dhidi ya
vyombo vyao vya ulinzi na usalama.
Alisema madai kuwa jeshi hilo limetumika na kuandikisha wananchi kwenye
kambi zao za jeshi visiwani Zanzibar si ya kweli na kama kuna mwenye
ushahidi auwasilishe ili ukweli ujulikane.
Dk Mwinyi alisema amesikitishwa na madai ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani
kuhusu masuala ya Muungano, Ally Abdallah Saleh kwamba Zanzibar
imetekwa na jeshi la Tanganyika kana kwamba nchi iko katika vita.
“Naomba nikujibu kwanza ili ufahamu kuwa hakuna jeshi la Tanganyika,
jeshi ni moja na ni la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Naomba
nimuelimishe kazi kubwa za jeshi ni ulinzi wa mipaka, ulinzi wa amani na
kutoa msaada kwa mamlaka za kiraia au vyombo vingine vya ulinzi na
usalama inapohitajika kufanya hivyo,” alisema.
Alisema inapotokea matukio makubwa kama shughuli ya uchaguzi, duniani
kote si Tanzania pekee, majeshi yote yanakuwa tayari kukabiliana na hali
yoyote na ndio maana askari wake wanakuwa kwenye sare za kombati.
Kuhusu madai ya kambi hiyo ya upinzani kuwa Jeshi limekuwa likitumika
kulazimisha Muungano, Dk Mwinyi alisema JWTZ ni kielelezo cha Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane mwaka 1964, jeshi ni moja
na kamwe halijawahi kulazimisha utawala, ila lipo hadi Zanzibar kwa
sababu ya kulinda mipaka ya Tanzania, na Zanzibar ni sehemu ya Tanzania.
“Tangu mwaka 1964 jeshi lina vikosi vyake Zanzibar na siku zote vikosi
hivi huwa na silaha, sasa tuna haja gani ya kupeleka wanajeshi na silaha
wakati miaka yote vyote viko huko? "Alihoji Dk Mwinyi.
Naye Naibu Waziri Masauni alisema hoja kwamba jeshi lilitumia mabavu Zanzibar na askari walikuwa ni wengi si ya kweli.
Alisema kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi, kila kituo cha uchaguzi
kinahitajika angalau askari wawili wakati Zanzibar kulikuwa na vituo vya
uchaguzi zaidi ya 3,000 na askari waliopo visiwani humo ni 5,000.
Alisema kwa hali ilivyokuwa askari wa Zanzibar walikuwa hawatoshi kwani
wangesambazwa wote wasingetosha kuweka ulinzi na kuhakikisha uchaguzi
unafanyika kwa utulivu na usalama.
Kuhusu madai kwamba Katiba imekiukwa, aliutaka upande wa upinzani
kujiuliza kati ya madai yao ya kumtaka Rais John Magufuli aingilie
mamlaka ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) au Polisi kulinda raia na
mali zao, kipi ni uvunjifu wa Katiba.
Alifafanua kuwa majukumu ya Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi ni kulinda usalama wa raia na mali zao hivyo bila kujali cheo au
utajiri wa mtu yeyote endapo atavunja sheria atachukuliwa hatua za
kisheria.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alisema uchaguzi wa
Zanzibar ulikamilika kwa usalama na kwamba pamoja na malalamiko ya
vichochoroni kuhusu uchaguzi huo, hakuna hata mmoja aliyefungua kesi
kupinga matokeo mahakamani.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ni ruhusa mtu asiporidhika na
matokeo ya uchaguzi, kufungua kesi ya kuyapinga, lakini tangu uchaguzi
huo umalizike hakuna mtu kutoka jimbo lolote visiwani humo aliyefungua
kesi.
Naye January alisema kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, Mahakama Kuu ya
Zanzibar ndio pekee yenye uwezo wa kusikiliza na kuamua masuala yote
yanayohusu uchaguzi wa Zanzibar.

0 comments:
Post a Comment