MIAKA
michache iliyopita, wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne ambayo
imeshapita, kuna jambo moja lilinishangaza sana. Jambo hili lilimhusu
Waziri wa Serikali hiyo na mlinzi wa benki.
Kilichotokea
ni kwamba Mheshimiwa Waziri alikwenda kwenye mashine ya kutolea fedha,
maarufu kama ATM, huenda kwa ajili ya kutoa fedha. Akiwa ndani ya kile
chumba akaanza kuzungumza na simu. Akazungumza na simu kwa muda mrefu,
hali iliyosababisha wateja waliokuwa wakiisubiri huduma hiyo kuanza
kulalamika na kumlazimu mlinzi kumuomba Waziri awapishe wateja wengine
waweze kupata huduma.
Hilo
halikumfurahisha Waziri yule na badala yake akaanza kumwuliza mlinzi
kama anajua yeye ni nani, kwa kuwa yeye kama Waziri ana mambo mengi ya
maana na alikuwa akizungumza na simu muhimu. Kwa huyo Waziri, suala la
kuzungumza kwenye chumba cha ATM na kuwanyima fursa wateja wengine kama
yeye kuipata huduma waliyokuwa wakiihitaji kwa wakati, halikuwa tatizo
kabisa.
Sakata
la Mheshimiwa Waziri na mlinzi wa benki liliripotiwa kwenye vyombo vya
habari na bahati mbaya mwisho wake ulikuwa wa kusikitisha, kwani mlinzi
alifukuzwa kazi kutokana na kutimiza majukumu yake. Baadhi ya watu
walipiga kelele, lakini hakuna kilichotokea. Sana sana, baba wa watu
akabaki bila kazi, huku akiwaza ataitunzaje familia yake iliyokuwa
ikimtegemea.
Sasa
juzi hapa hali hiyo imejirudia tena. Safari hii, hata hivyo,
imemhusisha Mke wa Mheshimiwa Waziri mwingine, ambaye alibishana na
askari wa usalama barabarani aliyekuwa akitimiza majukumu yake ya kazi
kwa kumweleza makosa ya barabarani aliyoyatenda. Badala ya kusikiliza
makosa yake na kuadhibiwa kwa kadiri ya matendo yake, mke huyu aliitumia
karata yake ya kupitia mgongo wa mumewe na kutoa kauli za kuudhi
zisizofaa kwa yule askari.
Kwa
mara ya kwanza katika kipindi kirefu sana, mambo yanaelekea kubadilika
na wale waliokuwa wakidhani wapo juu ya sheria, wanakumbushwa tena
kwamba Tanzania sio ya kwao peke yao.
Taarifa
zinasema kwamba Rais John Pombe Magufuli ameamuru askari wa usalama
barabarani aliyekuwa akifanya kazi yake na kuishia kutolewa maneno
yasiyofaa na Mke wa Waziri, apandishwe cheo. Vilevile, ameshamuonya
Waziri na Mke wake kuhusiana na tukio hilo, kwani hakuna mtu aliye juu
ya sheria.
Binafsi,
taarifa hiyo imenifurahisha sana. Tuseme tu ukweli kwamba Tanzania
ilikuwa nchi ya ajabu sana. Ilikuwa na matabaka makubwa sana kiasi cha
watu kuzungumzia kutaka hata kukimbilia kuishi nje ya nchi, kutokana na
kujiona hawathaminiwi, huku wengine wakitamba mitaani na kufukuzisha
watu kazi kana kwamba wao ndio wamiliki halali wa nchi hii.
Tanzania
ilifika mahali ambapo huyu askari wa usalama barabarani ambaye Rais
ameamua kumpandisha cheo, angekuwa katika hali ngumu sana. Kwanza
angetafutiwa zengwe, kisha angehamishwa kituo cha kazi na kupelekwa
kijijini huko kwenye kitengo cha kawaida kabisa. Wale aliowaudhi,
wangehakikisha kwamba jamaa harudi tena mjini, na anasahaulika kabisa.
Lakini
yote hii ni kutokana na ulimbukeni wa kada fulani kudhani wako juu ya
sheria na hawatakiwi kuguswa, huku sie akina yakhe tukiendelea kulipa
faini halali na wakati mwingine kuadhibiwa na askari mwenye hasira za
kutendwa na watu wa aina ya Mke wa Waziri.
Lakini
pamoja na taarifa njema hizi tulizozisikia mwishoni mwa wiki, bado tuna
safari ndefu sana. Bado wapo watu wanaodhani wako juu ya sheria,
hawatakiwi kuguswa na wanaruhusiwa kufanya chochote wanachojisikia
kukifanya kwa kuwa wao ni wao na hawawezi kulinganishwa na Watanzania
wengine.
Katika hili, naomba nizungumze na Mheshimiwa Rais na kumweleza maajabu ya Tanzania, ambayo bado hayajaandikwa kwenye Kitabu cha Guinness Book of Records.
Mheshimiwa
Rais, hivi unafahamu kwamba kwenye nchi hii mtu akiwa na gari lenye
nembo za Serikali, kama vile STK, huwa anavunja tu sheria za barabarani
na haulizwi chochote? Ataona watu wote tupo barabarani, tumesimama
kwenye foleni, tunasubiri nafasi yetu ifike ili tuendelee na safari,
lakini yupo radhi kupita hata njia za pembeni za watembea kwa miguu na
hataguswa. Eti ile nembo tu ya STK inamfanya awe juu ya sheria.
Mheshimiwa
Rais, wapo pia hawa wengine ambao wanadhani kwamba kutokana na vyeo
walivyonavyo, vyeo ambavyo aidha wewe ama watangulizi wao mmewapa, basi
hata wakifika maeneo ya huduma za umma, kama vile hospitali, hawahitaji
kufuata utaratibu wa kusimama kwenye foleni kama sisi wengine
tufanyavyo. Watafika, watawaona mmesimama, watapitiliza bila
kuwasemesha huku wakiwa wamekunja nyuso zao kwa hasira na ukijaribu
kuhoji, watakuuliza “unajua mimi ni nani?” Hawa pia wanadhani wako juu
ya sheria.
Mheshimiwa
Rais, wapo pia wale ambao wanajiona wapo ‘grade’ ya juu zaidi. Hawa
hufikia mahala pa kutumia magari ya umma, magari ambayo sisi tunayalipia
kodi ili yanunuliwe, yakarabatiwe na yajazwe mafuta, lakini wao kuamua
kuyatumia kwa mambo yao binafsi. Magari haya yatakwenda sokoni kununua
mchicha na vitunguu, yatapaki saluni kumsubiri ‘mama’ ajiweke vizuri na
yatapaki baa kusubiri bosi apate mapumziko ya kutosha, hata kama ni hadi
usiku wa manane. Yaani sisi tunakatwa kodi ili wao watumbue maisha,
kwani wanadhani kwamba wako juu ya sheria.
Mheshimiwa
Rais, wapo na wale ambao hata tukiwa kwenye foleni za benki, basi wao
wataingia na kupitiliza ili wahudumiwe kwanza, kana kwamba wengine
tuliosimama pale ni milingoti ya TANESCO na hatuna mambo mengine ya
kufanya. Ukihoji, utasikia: “kwani wewe hujui mimi ni nani? Nina mambo
muhimu ya kitaifa ya kufanya.” Unabaki unajiuliza, hivi kumbe kuna watu
na WATU. Kwa kila kitu, wao wapo juu ya sheria.
Naomba
tu niseme kwamba hali hii ilikera kiasi kwamba tukaizoea na ndio maana
hata Mke wa Waziri alipotoa maneno yasiyofaa kwa askari wa usalama
barabarani, hakuna aliyejua kwamba askari yule angepandishwa cheo na
Waziri kuonywa. Sana sana, tulikuwa na uhakika kwamba hili litasambazwa
sana kwenye mitandao ya jamii, huku wale wanaotukana askari kwamba
wanachokitaka ni rushwa tu, wakiendeleza kauli hizo za kuudhi.
Watu
walijiona kwamba wao ndio Watanzania halisi na wengine ni wa
kusingiziwa. Watu walijiona kwamba wao ndiyo pekee wenye haki miliki ya
nchi. Watu walijiona kwamba wao wako juu ya sheria. Mheshimiwa Rais,
naomba nikuhakikishie kwamba watu hao bado wapo wengi…

0 comments:
Post a Comment