Tuesday, 12 April 2016

Takukuru yafuatilia Sakata la Panama Papers

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishna Valentino Mlowola

Wakati viongozi, wafanyabiashara na makampuni makubwa barani Afrika yakitajwa kwenye kashfa ya ukwepaji kodi ya Panama papers, hapa nchini Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) imesema kuwa inafuatilia ripoti hiyo kubaini kama kuna watanzania waliohusika.

Kashfa hiyo ambayo had hivi sasa imekwisha tiskisa sehemu mbalimbali za dunia inahusisha nyaraka zilizoibuliwa na mtandao wa waandishi wa habari ambazo zinawafichua watu maarufu duniani wakiwamo wakuu wa nchi 12 walioko madarakani na waliostaafu pamoja na familia na rafiki zao wa karibu ambao wamenufaika na ukwepaji kodi.

Wakati nchi za watu maarufu kutoka barani Afrika kama Kenya, Afrika Kusini,Nigeria, Zimbabwe, Angola, Congo na Rwanda zikitajwa kwenye kashfa hiyo hakuna mtanzania wala kampuni ya hapa nchini inayohusishwa na sakata hilo.

Lakini Mkurugenzi wa Takukuru Kamishna Valentino Mlowola alifunguka kuwa Taasisi yake bado inafuatilia kwa kina taarifa hiyo ili kujiridhisha kama ni kweli hakuna Mtanzania yeyote anayehusika.
Alisema endapo itabainika kuwapo kwa watanzania kwenye kashfa hiyo watachukuliwa hatua kulingana na sheria zilizopo.

"Ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba tunaendelea kuangalia ripoti na tukibaini uwepo wa watanzania mambo mengine yatafuata ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua kulingana na sheria zetu za hapa nchini", alisema Mlowola

0 comments:

Post a Comment