MWILI wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na
Utumishi wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Amatus Liyumba (68) unatarajiwa
kuagwa leo na kusafirishwa kwenda Morogoro kwa mazishi.
Mtoto
wa marehemu, Moses Amatus, akizungumza na waandishi wa habari jana
jijini Dar es Salaam jana, alisema mipango na taratibu za mazishi ya
marehemu inaendelea kufanyika kati ya ndugu na jamaa.
Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida Nipashe ilipofika nyumbani
kwa marehemu, haikushuhudia uwepo wa kiongozi yeyote wa serikali, licha
ya marehemu kuwa mmoja wa watu ambao walikuwa na wadhifa mkubwa katika
utumishi wa umma.
Liyumba alifariki dunia juzi katika hospitali ya Aga Khan, Dar es
Salaam baada ya kulazwa mwishoni mwa wiki kutokana na kuugua ugonjwa wa
kisukari kwa muda mrefu.
“Baba alikuwa akiugua ugonjwa huo kwa muda mrefu lakini hivi karibuni
alizidiwa ghafla, hivyo kumpeleka hospitalini kwa matibabu zaidi ingawa
alifariki dunai baada ya siku mbili tangu kulazwa,”.
Liyumba lizaliwa mwaka 1948, ameacha watoto saba na kwamba hajaacha
mjane kutokana na mke wake kufariki miaka zaidi ya 10 iliyopita.
“Marehemu hakubahatika kuoa tena baada ya mke wake kufariki dunia mwaka 2005,” alisema Moses.
Liyumba aliwahi kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
mwaka 2009, kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia
serikali hasara ya Sh. bilioni 221.
Hata hivyo, alishinda kesi hiyo baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha tuhuma hizo.
Januari 27, 2009 Liyumba na aliyekuwa Meneja Miradi wa BoT,
Deogratius Kweka, walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuidhinisha
ujenzi wa majengo pacha ya BoT bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi.
Kabla ya kuanza kusikiliza ushahidi wa kesi hiyo, upande wa mashtaka
ulimwachia Kweka na uliwasilisha mashahidi wanane, wakiwamo wakurugenzi
wa Bodi ya BoT na vielelezo mbalimbali.
Mahakama hiyo baada ya kusikiliza pande zote, Mei 24, 2010 ilimhukumu
Liyumba kwenda jela miaka mwili, baada ya kukutwa na hatia ya kutumia
madaraka vibaya akiwa mtumishi na mkurugenzi wa BoT.
Imeandikwa na Christina Mwakangale na Abraham Ntambara

0 comments:
Post a Comment