Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amekumbana na joto la Mbeya baada ya
meya wa jiji hilo, Mchungaji David Mwashilindi na madiwani wake 34
kususia kikao chake cha kujitambulisha kwa wananchi, baada ya kudaiwa
kwenda kukagua Soko la Mwanjelwa bila kumpa taarifa yoyote meya wa jiji
hilo.
Meya alifikia uamuzi huo ndani ya ukumbi wa Mkapa muda mfupi kabla ya
Makalla kuanza kuzungumza na watumishi wa jiji, wananchi, wazee maarufu,
viongozi wa dini na machifu ambapo Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Nyirembe
Sabi alimkaribisha Meya Mwashilindi kuzungumza chochote kwa niaba ya
madiwani wake.
Hata hivyo, Meya Mwashilindi alipochukua kipaza sauti alisema: “Mkuu wa
Mkoa wa Mbeya, nakumbuka kwa mara ya kwanza kukutana na wewe
tulizungumza kwamba tufanye kazi, siasa zimekwisha. Lakini masikitiko
yangu ni kwamba leo hii umekwenda Soko la Mwanjelwa bila ya mimi mwenye
jiji kupewa taarifa yoyote wala madiwani wangu. Sasa hiki kikao
hakinihusu hivyo muendelee na kikao chenu.”
Baada ya kusema maneno hayo alikabidhi kipaza sauti kwa mkuu wa wilaya,
kisha akachukua nyaraka zake akainuka pamoja na madiwani wote kupitia
Chadema na kutoka ukumbini huku wakisikika wakisema, ‘hizi ni siasa
ambazo tulizikataa, lakini wanatulazimisha kuendesha siasa. Hatuwezi
kupuuzwa kwa kiasi hiki.”
Mkuu wa Wilaya, Mnasa alisema anaamini taratibu na ratiba yote ilipangwa
vizuri hivyo hawaoni sababu ya madai ya madiwani hao kwamba
hawakushirikishwa kwenye ziara hiyo, wao kama wawakilishi wa Rais
hawaangalii siasa, bali wanaangalia uchapakazi na siyo masuala ya siasa.
Akizungumzia kitendo cha meya na madiwani wake kususia kikao hicho,
Makalla alisema ‘Nashangazwa na uamuzi wa madiwani hawa kwa kitendo
hiki, kwani siku ile nilipotembelea Shule ya Sekondari Iyunga, nilisema
kwamba Aprili 20 ambayo ndiyo leo (jana) nitakuwa na ziara ya jiji na
kabla ya kikao nitataka kutembelea Soko la Mwanjelwa,” alisema Makalla.
Alisema suala la meya na madiwani wake kutoshirikishwa kwenye ziara ya
kwenda Soko la Mwanjelwa halimhusu, kwani mwenye wajibu wa kupeana
taarifa ni kwenye ngazi ya halmashauri ya jiji, lakini siyo yeye
(Makalla).
“Jamani mimi sijaja kufanya siasa nimekuja kufanya kazi ya wananchi na
nilishatahadharisha jambo hili, sasa kwa kitendo hiki ndiyo siasa na
wananilazimisha kufanya siasa, lakini wao ndiyo watahukumiwa na
wananchi. Na ninasema kama Mola ataendelea kunilinda kubaki katika mkoa
mwaka 2020 nitakwenda kuwaambia hiki kinachofanyika sasa na wawakilishi
wao,” alisema Makalla.
Awali Makalla akiwa katika Soko la Mwanjelwa alinusa harufu ya ufisadi
kwenye soko hilo na kuagiza vyombo vya ulinzi na usalama mkoa huo,
kufanya uchunguzi ndani ya wiki nne wa uhalali wa fedha kiasi cha Sh22.9
bilioni iliyotumika katika ujenzi huo ukiwa ni mkopo kutoka Benki ya
CRDB.
Makalla alitoa agizo hilo jana mchana baada ya kutembelea soko hilo na
kuzungumza na wafanyabiashara wa jijini hapa, ambao walimueleza
wanashindwa kumudu gharama ya upangaji ya vyumba vya biashara ambayo
inaanzia kiasi cha Sh500,000 kwa chumba kimoja kwa mwezi, ndiyo maana
hawataki kuingia ndani ya soko hilo.
Mwenyekiti wa soko hilo, Peter Chacha alimueleza Makalla kwamba
wasipokuwa makini soko hilo litabaki gofu, kwani wafanyabiashara
hawataki kuingia kwa kuogopa gharama kubwa ya vyumba hivyo, alimuomba
afanye awezalo kukaa chini na uongozi wa benki ambao unadai fedha zao
kwa jiji na kuona namna ya kupunguziwa gharama hiyo.
“Ni kweli wenzetu jiji, wametingwa na deni la mkopo kutoka Benki ya
CRDB, ndiyo maana wamekuja kutubana sisi wafanyabiashara kwa kutupangia
chumba kuanzia Sh500, 000 hadi Sh 800,000, kitu ambacho hatuwezi kumudu
hata kidogo,”alisema Chacha
Baada ya kusikiliza kilio cha wafanyabiashara hao, Makalla alisema kiasi
cha Sh22.9 bilioni iliyotumika kwenye ujenzi wa soko hilo haiendani na
thamani yake, hivyo vyombo vya dola vikiongozwa na Kamanda wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mbeya, wanafanya
uchunguzi wa kina na kuwanasaka wale wote waliohusika kwenye mchakato
mzima wa ujenzi wa soko hilo.
“Nataka kupata taarifa ya mchanganuo mzima wa namna ya fedha
ilivyokopwa, ilivyotumika na mkataba wake ulivyokuwa ndani ya wiki nne,
taarifa hii niipokee na wale watakaobainisha kufuja fedha watapelekwa
mahakamani kwa mujibu wa sheria.
"Kwenye hili, kuna watu waliotufikisha hapa, Sh22.9 bilioni iliyotumika
kwenye ujenzi huu haiendani na ujenzi wa soko hili, kuanzia muda
uliotumika na gharama ya kodi ya upangishaji wa vyumba siyo rafiki ni
kubwa mno, hivyo jiji na CRDB mkae muone namna ya kupunguza gharama
hiyo, kwani hali ilivyo sasa lile soko litabaki gofu."

0 comments:
Post a Comment