Hatimaye taarifa ya utekelezaji wa mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi
Enterprises, iliyoshinda zabuni mwaka 2011 ya kufunga mashine za
kuchukua alama za vidole katika vituo vya Polisi vya wilaya nchi nzima
kwa gharama ya Sh bilioni 37, umetua ndani ya Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Hesabu za Serikali (PAC) na kuanza kujadiliwa.
Akizungumza jana bungeni, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hilaly
alisema taarifa ya utekelezaji wa mkataba huo, ilifikishwa bungeni juzi
na jana asubuhi wamepewa na wakaanza kuujadili papo hapo.
“Wametuletea taarifa ya utekelezaji wa mkataba huo leo asubuhi (jana),
ila taarifa hiyo ilifika bungeni jana (juzi), na sisi kamati tumekaa
asubuhi kuijadili kama tulivyokubaliana wakati wa vikao vya kamati mjini
Dar es Salaam na tutatoa taarifa ya maamuzi ya kamati,” alisema Aeshi
ambaye ni Mbunge wa Sumbawanga Mjini.
Akizungumza baada ya kuahirisha kikao cha kamati hiyo jana jioni, Aeshi
alisema hawajafikia maamuzi na kwamba leo wataendelea kujadili taarifa
hiyo na mchana watatoa maazimio ya kamati.
“Tumeahirisha kikao hadi kesho (leo) na bado tunapitia taarifa hiyo na
kama kamati itaona haja ya kuwaita tena jeshi hilo kutoa maelezo,
tutajua baada ya kufikia maamuzi,” alisema Aeshi na kuongeza kuwa kwa
sasa wanachambua taarifa hiyo na iwapo wataona kuna haja pia ya kuutaka
mkataba huo watatoa maelekezo.
Awali, Aprili 5, mwaka huu mjini Dar es Salaam, kamati hiyo ilitoa siku
saba kuanzia siku hiyo kwa Jeshi la Polisi nchini, kupeleka mkataba
walioingia baina yao na Kampuni ya Lugumi iliyopewa zabuni ya kufunga
mashine 108 katika vituo tajwa nchini, ila hadi sasa ni vituo 14 tu
ndivyo vilivyofungwa mashine hizo.
Hatua hiyo ilikuja baada ya kamati hiyo kukutana na jeshi hilo kupitia
taarifa ya hesabu za jeshi hilo za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kubainika kuwa
na ukiukwaji wa utekelezaji wa mkataba huo.
Ukiukwaji wa utekelezaji wa mkataba huo mwingine ni pamoja na kampuni
hiyo kulipwa asilimia 99 ya fedha zote za mkataba huo wenye thamani ya
Sh bilioni 37, huku kazi iliyofanywa ni chini ya robo.
“Ukiangalia kazi iliyofanywa tangu mwaka 2011 hadi leo ni kidogo na pesa
hawa kampuni wameshachukua asilimia 99, sasa tumewaagiza watuletee huo
mkataba ndani ya wiki moja walioingia na kampuni hiyo ili tuupitie,”
alisema Aeshi wakati wa vikao vya Dar es Salaam.
Hata hivyo, baada ya maagizo hayo, taarifa hiyo ya utekelezaji
haikuwasilishwa kwenye kamati hiyo ndani ya muda uliokubaliwa na Aeshi
alisema siku zote wamekuwa wakitoa maagizo kwa mdomo na taasisi nyingi
zimekuwa zikitekeleza.
Aliongeza ila hilo la mkataba wa Lugumi lilikuwa tabu kutekelezwa hadi
kamati hiyo, ilipochukua hatua za kukumbushia kwa kuandika maelezo.
Hata hivyo, baada ya taarifa za mkataba huo,zilisambaa habari kwenye
vyombo vya habari kuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo ni Mbunge wa
Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), Said Lugumi na vigogo wengine.
Kutokana na sakata hilo, mbunge huyo alikanusha kuhusika kwake na kusema
ni kweli kwamba ana urafiki wa kawaida na Said Lugumi na kusisitiza
kwamba hahusiki kwa njia yoyote na kampuni hiyo.
“Kwanza kabisa mimi si mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo, hilo ni jambo
la msingi kabisa watu waelewe na sijawahi kufanya biashara yoyote na
Lugumi. Said Lugumi ambaye ni mmiliki wa kampuni hiyo tunafahamiana naye
na ni rafiki yangu,” alisema Ridhiwani.

0 comments:
Post a Comment