Thursday, 21 April 2016

Bwawa la Mtera sasa lajaa pomoni, maji yatiririshwa

BWAWA la kuzalisha umeme kwa maji la Kidatu mkoani Morogoro limezidiwa na maji na kulazimu Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kushirikiana na Serikali kufungulia maji yaliyozidi na kuanza kupita katika geti kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Hatua hiyo imetokana na iwapo wataacha yaendelee kutoka bila kuyadhibiti taratibu itasababisha uharibifu wa miundombinu na kuhatarisha maisha ya watu. Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema maji ya bwawa hilo yamekuwa mengi hivyo yanaweza kuathiri usalama wa bwawa, kwani limetengenezwa kupokea kiasi fulani cha maji hivyo yakizidi presha yanagonga kwenye kingo na yanaweza kusababisha maafa.
Mramba alisema pia maji yanapotoka katika bwawa hilo na kurudi mtoni yanaweza kusababisha madhara kwa wananchi wanaofanya shughuli mbalimbali kwenye mto, hivyo ni vema kuyadhibiti.
Alisema bwawa hilo limefurika maji licha ya kuzuia maji ya bwawa la Mtera yanayoingia humo kufungwa kwa zaidi ya wiki mbili na mashine zote nne za kuzalisha umeme kuendelea kuzalisha umeme kwa kiwango cha juu.
Mramba alikuwa akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen na kueleza kufungulia maji hayo ni makubaliano kati ya serikali na wataalamu wa shirika hilo ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
Alisema kiwango cha juu za bwawa hilo kuhifadhi maji ni mita za ujazo 450, lakini mpaka juzi ilikuwa imefikiwa mita za ujazo 450.49 hivyo kwa ajili ya masuala ya usalama kiasi cha maji kilichozidi lazima kiondolewe.
Mramba alisema kwa mvua zinazoendelea kunyesha zimeongeza maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme kwani katika bwawa la kuzalisha umeme la Mtera, maji yameongezeka na kufikia mita za ujazo 697.14 wakati kiwango chake cha juu ni mita za ujazo 698.
Mwezi uliopita, Rais John Magufuli wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme wa Megawati 240 Kinyerezi II aliwataka Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, kuhifadhi maji ya mvua ili asisikie wakati wa ukame kuwa mitambo ya kuzalisha umeme imeishiwa maji.

0 comments:

Post a Comment