Friday, 11 March 2016

Yanga yatua Kigali, yatikisa jiji

                                 Wachezaji wa Yanga wakishangilia moja ya mabao katika ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika Yanga, jana waliwasili Kigali, Rwanda na kutamba kuibuka na ushindi dhidi ya APR katika mchezo utakaofanyika kesho.
Ujio wa Yanga iliyowasili asubuhi, umekuwa gumzo katika Jiji la Kigali kutokana na mabingwa hao wa Tanzania kuonekana kuwa tishio katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Mashabiki wamekuwa wakiizungumzia mno mechi hiyo, hasa `uzito’ wa Yanga yenye nyota waliowahi kuichezea APR, Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite.
Aidha, mara baada ya kikosi cha Yanga kutua kwa ndege kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Kanombe uliopo kilometa chache kutoka Uwanja wa Amahoro, eneo la Kicukiro jijini Kigali, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm aliwaambia waandishi wa habari kuwa, ushindi ndio uliowapeleka nchini humo.
“Tunataka kushinda na hicho ndicho kilichotuleta. Lakini tunajua APR ni timu nzuri, tunaheshimu hilo. Lakini hakika tunataka kutengeneza mazingira bora ya mechi ya marudiano kule Dar es Salaam.
“Kushinda huku (Kigali), kutafanya tuwe katika nafasi nzuri ya kufanya vyema zaidi,” alisema Pluijm ambaye amekwenda na nyota wake wote, isipokuwa Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Malimi Busungu na Benedicto Tinocco.
Haroub alikuwa akisumbuliwa na majeruhi, ambapo bado hajawa imara hivyo, alikosa pia katika michezo kadhaa ya Ligi Kuu huku mpinzani wake katika namba Vincent Bossou akionekana kung’ara zaidi katika nafasi hiyo.
Mchezaji huyo alitemwa pia katika kikosi kilichoitwa na Kocha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ Charles Mkwasa. Kwa Busungu naye pia hakuwepo katika kikosi kilichocheza dhidi ya African Sports ya Tanga Jumanne na kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Taifa.
Mechi hiyo inatarajiwa kuchezeshwa na waamuzi kutoka Malawi kwenye Uwanja wa Amahoro. Hao ni Duncan Lengani anatarajiwa kupuliza filimbi, wakati washika vibendera ni Clemence Kanduku na Jonizio Luwizi.
Mchezo wa marudiano utachezwa wiki moja baadaye Dar es Salaam, na marefa wa Shelisheli, Bernard Camille (katikati) na pemebeni watakuwapo Eldrick Adelaide na Gerard Pool.
Yanga imefikia katika Hoteli ya kifahari ya Mirror mjini Kigali, wakati jana jioni walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa nyasi wa bandia wa Shirikisho ya Soka la Rwanda (FERWAFA).

0 comments:

Post a Comment