
- Ni kuhusiana na zile za rushwa zinazowakabili wabunge wanne wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliofikishwa mahakama ya hakimu mkazi kisutu hivi karibuni
SIKU chache baada ya wabunge wanne kupandishwa kizimbani kutokana na kashfa za rushwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema chombo hicho cha kutunga sheria, kwa sasa kinakabiliwa na mambo mazito ambayo hayawezi kuzungumnzika nje ya muhimili huo.
Kauli hiyo ya Ndugai imekuja ikiwa ni takriban miezi minne tangu kuzinduliwa rasmi kwa Bunge la 11 na kufunguliwa na Rais John Magufuli Novemba 20, mwaka jana alipolihutubia na pamoja na mambo mengine aliapa kupambana na wala rushwa akisema “nitatumbua majipu yote." Wabunge wanne ambao wamefikishwa mahakamani ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwamo Richard Ndassa (Sumve), Victor Mwambalaswa (Lupa), Kangi Lugola (Mwibara) na Suleiman Sadiq maarufu Murad wa Mvomero.
NDUGAI Jana Ndugai aliliambia Nipashe kwa kifupi kwamba: “Haya siyo mambo ya kuongelea Dar es Salaam.
Nitayazungumza bungeni kwenye kikao cha kwanza tu.” Aliongeza: “Haya ni mambo mazito na ufafanuzi wake nitautoa bungeni, kwa sasa siwezi kuongea chochote, wewe niache tu.”
HALI ILIVYO
Bunge la 11, ni kati ya Mabunge ambayo ndani ya muda mfupi yamekabiliwa na kashfa nzito ambazo zimeutia doa mhimili huo.
Mbali na tuhuma hizo, hadi sasa Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na ile ya Hesabu za Serikali (PAC), hazijapata wenyeviti kutokana na kambi rasmi ya upinzani bungeni kuisusia kutokana na kutoridhishwa na namna ambavyo spika alipanga wajumbe wa kamati hizo.
Pia, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), nayo ipo kwenye mgogoro wa kikanuni kutokana kile ambacho baadhi ya wabunge wakiwamo wa CCM, kudai imepewa mamlaka ya kukagua hesabu za mashirika ya umma, jambo ambalo ni kinyume cha kanuni.
Mabunge yanayofuata mfumo wa Jumuiya ya Madola, kamati zinazosimamia hesabu za serikali, zinatakiwa ziongozwe na wenyeviti kutoka kambi ya upinzani.
Hivyo, suala la kamati hizo kuendelea kutopata wenyeviti, ni mtihani mwingine mzito kwa Ndugai, huku ile ya PIC ikitarajiwa kuleta mgongano zaidi wa kikanuni.
TUHUMA ZA RUSHWA
Wabunge ambao wamepandishwa kizimbani wanakabiliwa na tuhuma za kushawishi na kuomba rushwa. Lugola, Mwambalaswa na Murad, wao wameshtakiwa kwa tuhuma za kushawishi na kuomba rushwa ya Sh. milioni 30 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.
Wabunge hawa ni wajumbe wa LAAC na Lugola ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, ambayo haina mwenyekiti baada ya Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni kususia uteuzi wa wajumbe hasa wanaotoka vyama vya upinzani.
Kwa upande wake, Ndassa anatuhumiwa kuomba rushwa ya Sh. milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Felichismi Mramba.
Pia, Ndassa ambaye ni mjumbe wa PIC, anadaiwa kuomba rushwa ya kupata bure huduma ya umeme kwake (mbunge huyo), ndugu yake na rafiki wa ndugu yake.
BUNGE LA 10
Tuhuma za rushwa kwa wabunge hasa wajumbe wa LAAC, hazijaanzia kwenye Bunge hili, kwani mwaka 2012, mbunge wa Bahi (CCM), Omar Badweli, alipandishwa kizimbani kwa tuhuma mbili za kushawishi kuomba rushwa ya Sh. milioni nane kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Sipora Liana.
Tuhuma ya pili ni kupokea rushwa ya Sh. milioni moja. Hata hivyo, Badwel alishinda kesi hiyo.
Mwaka huo huo, wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, walituhumiwa kuomba na kula rushwa, hivyo kumfanya aliyekuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuivunja kamati hiyo pasipo kuchukua hatua za ziada.
Wabunge hao walituhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa kampuni za mafuta ili kuipigia debe menejimenti ya Tanesco. Baada ya malumbano ndani ya Bunge, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu, aliwataja wabunge sita wa CCM waliojihusisha na vitendo vya rushwa kuwa ni Munde Tambwe, Sarah Msafiri, Mariam Kisangi wa Viti Maalum, Yusuf Nassir (Korogwe Mjini) na Charles Mwijage wa Muleba Kaskazini.
Tambwe na Msafiri walitajwa kuwa na tenda ya kuiuzia Tanesco matairi na kwamba hawajawahi kutangaza maslahi yao katika jambo hilo kwenye kamati zao.
Mwijage ambaye sasa ni Waziri wa Viwanda na Biashara, alitajwa kuwa mtaalam mwelekezi wa Kampuni ya Puma Energy iliyokuwa imepewa zabuni ya kuiuzia mafuta Tanesco, hivyo alikuwa na mgogoro wa kimaslahi.
Pia, LAAC ambayo ilikuwa inaongozwa na Augustine Mrema pamoja na PAC (wakati huo POAC), iliyokuwa inaongozwa na Kabwe Zitto, nazo baadhi ya wajumbe wake walikuwa wakitajwa kujihusisha na vitendo vya rushwa. Wabunge hao kwa nyakati tofauti walikanusha tuhuma hizo.
0 comments:
Post a Comment