Monday, 14 March 2016

DC ataka walimu watatue changamoto

       Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema akimpima uzito mtoto wa miezi 18, Shafii Haji, mkazi wa Kibugumo Darajani, kama ishara ya kuzindua kambi ya upimaji afya kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, iliyofadhiliwa na Umoja wa Watu wa Bengali na India waishio nchini (Bango Sangho), katika Shule ya Msingi Kibugumo, Kigamboni, Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mratibu wa kambi hiyo kutoka Kliniki ya Al Hilal, Dk Ali Mzige na Muuguzi wa Zahanati ya Kibugumo, Agnes Mokiwa (kulia). (Picha na Fadhili Akida).
MKUU wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema amewataka walimu wa wilaya hiyo kuwa wabunifu ili kutatua baadhi ya matatizo wanayoweza kuyashughulikia, badala ya kusubiri msaada kutoka kwenye taasisi binafsi au Serikalini.
Alisema hayo juzi wakati wa hafla ya kukabidhi msaada wa kompyuta, printa, tangi la maji la lita 5000, umeme, madarasa saba yaliyofanyiwa ukarabati, madaftari na kalamu katika Shule ya Msingi Kibugumo iliyopo Kigamboni. Hafla hiyo ilienda sambamba na utoaji huduma ya kupima afya bure kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano.
Msaada huo ulitolewa na Umoja wa Watu kutoka Bengali, India wanaoishi nchini (Bango Sangho). Mjema alisema, wilaya yake ina upungufu mkubwa katika sekta ya elimu, hivyo ni vema matatizo mengine walimu wakawa wanabuni njia mpya za kuyamaliza.
“Wilaya yetu inahitaji madarasa 2,891 na madawati 28,000, hivyo niwasihi walimu muda mwingine mnatakiwa kuwa wabunifu ili kumaliza changamoto ndogo zilizo ndani ya uwezo wenu,” alisema.
Pia, aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kuwa na utaratibu wa kupima afya mara kwa mara ili waweze kutambua magonjwa waliyonayo kabla hayajaanza kuwasumbua na hata wengine kupoteza maisha.
Aliwashukuru Bango Sangho kwa msaada huo na kuutaka umoja huo kupeleka huduma hiyo ya kupima afya kwa watoto walio chini ya miaka mitano kila baada ya miezi mitatu. Umoja huo kupitia Mwenyekiti wake, Kunal Banerjee ulisema uliamua kutoa msaada huo kwa shule ya Kibugumo kwa kutambua umuhimu wa afya na elimu bora kwa maendeleo ya sasa na baadae kwa taifa.

0 comments:

Post a Comment