Mzimu wa kuzuia shughuli za Bunge kuonyeshwa moja kwa moja na vituo vya
televisheni uliopachikwa jina la ‘Bunge Live’, umeendelea kumwandama
Waziri wa Habari, Nape Nnauye baada ya juzi kupokewa kwa kelele kiasi
cha kushindwa kuhutubia wapenzi wa muziki jijini Mwanza.
Nape alitangaza uamuzi wa kusitisha kurusha moja kwa moja baadhi ya
shughuli za Bunge, akisema Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC)
linashindwa kumudu gharama, lakini wabunge, hasa kutoka vyama vya
upinzani wamepinga hatua hiyo wakisema inawanyima wananchi haki yao ya
kikatiba ya kupata habari kuhusu chombo chao cha kutunga sheria.
Lakini Serikali imeshikilia msimamo wake, ikitoa sababu tofauti na
kwenda mbali zaidi kuzuia vituo binafsi vya televisheni kurusha
matangazo, huku TBC1 ikirusha kipindi cha maswali na majibu pekee
ikielezwa kuwa huo ni uamuzi uliopitishwa katika Bunge la 10.
Juzi, Nape aliyekuwa mgeni rasmi katika tamasha la Jembeka Festival
lililofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, alipokewa na kelele za
maneno “Bunge Live” wakati akikaribishwa kuhutubia mamia ya wapenzi wa
burudani waliohudhuria tamasha hilo, ambalo lilijumuisha wasanii nyota
kama Shaffer Chimere Smith a.k.a Ne-Yo kutoka Marekani na Diamond
Platnum.
Baada ya mkurugenzi wa kampuni ya Jembe ni Jembe, Sebastian Ndege
kumkaribisha waziri huyo kuzungumza na wananchi hao, Nape alisimama
lakini akapokewa kwa kelele.
“Bunge live, Bunge live, Bunge live,” walipiga kelele mashabiki waliohudhuria tamasha hilo.
Kelele za “Bunge Live” zilisababisha Waziri Nape kushindwa kuhutubia na
kulazimika kuketi chini na Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula
alisimama kujaribu kuokoa jahazi, lakini naye akakumbana na kimbunga cha
sauti za wananchi walioamua kulitaja jina la mbunge wa zamani wa jimbo
hilo, Ezekia Wenje.
“Wenje, Wenje, Wenje,” wananchi hao waliimba kwa sauti wakati Mabula akijaribu kuwatuliza ili Nape ahutubie.
Akizungumzia tukio hilo, Nape alisema wananchi waliompigia kelele za
“Bunge Live” walisukumwa na masuala ya kisiasa, ndiyo maana aliepuka
kuendelea kuzungumza ili kutochafua hali ya hewa uwanjani.
“Pale uwanjani tulikwenda kwa ajili ya burudani, sasa baada ya kuona
wananchi wanaanza kuleta masuala ya kisiasa nikaona ni busara kuacha
kuhutubia. kuepusha shari,” alisema Nape.
Pamoja na Nape, tamasha hilo pia lilihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba, Mkuu wa Mkoa
wa Mwanza, John Mongella na Mabula.
Ukiachilia mbali dosari hizo, tamasha hilo lilikonga nyoyo za wapenzi wa
sanaa ya muziki waliokesha uwanjani hapo hadi saa 11:00 alfajiri
wakiburudishwa na wasanii nguli.
Wasanii wengine waliopata nafasi ya kutumbuiza ni Juma Nature, Ney wa Mitego, Ruby na Fid Q.
0 comments:
Post a Comment