JUMLA ya wanachama wanne kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Manispaa ya Singida, wamejitokeza kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Jimbo hilo katika uchaguzi utakaofanyika Aprili 17, mwaka huu.
Ofisa Habari wa chama hicho Jimbo la Manispaa ya Singida, Sylvester Mirambo aliwataja waliochukua fomu na kutia nia ya kugombea kuwa ni pamoja na Diwani wa Viti Maalumu Manispaa ya Singida, Josephine Lemoyani.
Mirambo aliwataja wanachama wengine wanaowania nafasi hiyo kuwa ni Juma Saidi Ng’wadi, Lumbael Mjengi na Yassin Kaali. Kwa mujibu wa Ofisa Habari huyo, nafasi hiyo ipo wazi baada ya aliyekuwa Mwenyekiti, John Kumalija kung’olewa madarakani na uongozi wa ngazi ya juu kutokana na kile walichodai kutoridhishwa na utendaji wake wa kazi.
Wakati huo huo, Mirambo alisema kuwa kutakuwa na uchaguzi wa kumchagua mwanachama atakayeziba pengo la nafasi ya Katibu Vijana wa chama hicho (Bavicha) ambapo watu watatu, akiwemo yeye, wamejitokeza. Wengine ni Michael Mtaza na Amosi Gwau.
Aidha, alisema kutakuwepo na uchaguzi kwa ajili ya kujaza nafasi kwenye Baraza la Wanawake (Bawacha).
“Nafasi hizo ni Mwenyekiti, Katibu, Katibu Mwenezi, Mweka Hazina na wajumbe watano. Hata hivyo, hadi sasa hakuna mwanamke aliyejitokeza kuomba”.
Alisema kuwa kutokana na tarehe ya mwisho ya kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi hizo kuwa Aprili 6 mwaka huu, anatarajia wanawake wataweza kujitokeza kuchukua fomu kabla ya muda huo kumalizika.
Alisema kuwa mchujo wa wagombea utafanyika Aprili 6 mwaka huu na uchaguzi unatarajiwa kufanyika Aprili 17 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment