
JIJI la Mwanza ni miongoni mwa halmashauri nchini ambazo zina rekodi mbaya ya ufujaji wa fedha na hivyo kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, imeelezwa.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella aliyasema hayo jana jijini Mwanza wakati alipokuwa akizungumza na watendaji na watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwenye ziara yake ya kwanza ya kikazi.
Mongella alisema kutokana na hali hiyo imewafanya baadhi ya watumishi kutoka maeneo mengine ya nchi kufanya mbinu na kuhamishiwa katika jiji hilo ili waendeleze kile alichokiita kuwa ni utafunaji wa fedha za halmashauri.
“Katika halmashauri zinazoonekana ni kichwa cha mwendawazimu katika suala la kufuja fedha ni pamoja na jiji la Mwanza,” alisema na kuongeza, “Nasema nikimbaini kwa sasa mtu anayetafuna fedha za jiji nitashughulika naye.”
Alisema ni vyema watu wakatekeleza majukumu yao ya kazi kwa kufuata sheria na kwamba katika suala la matumizi mabaya ya fedha hataendelea kuona mtumishi akitumia fedha vibaya ingawa hakufafanua ni kiasi gani cha fedha kilichotafunwa hadi sasa.
Aliwataka watumishi na wafanyakazi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kufanya kazi kwa kadri ya taaluma zao na kwamba Serikali itamlinda na kumthamini mtumishi atakayeleta tija katika kuwahudumia wananchi.
“Hakuna kuoneana haya kwa mtumishi ambaye hawajibiki vyema kwa wananchi, na katika hili Rais ametuonesha mfano kila siku namna bora ya kuwahudumia wananchi wetu,” alifafanua.
Aliwataka watumishi wote kufanya kazi kwa uadilifu ili kutekeleza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi kulingana na kiapo alichoapa na kwamba atakayefanya kazi kwa tija serikali itamlinda.
0 comments:
Post a Comment