Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela juzi alivamia kituo cha Radio Ebony Fm cha mjini Iringa na kuamuru kukamatwa kwa watangazaji wawili waliomuigiza sauti yake, kuadhimisha siku ya wajinga duniani.
Kwa siku kadhaa, Kasesela amekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii kutokana kusambaa kwa picha zinazomuonyesha akitekeleza majukumu yake.
Miongoni mwa picha hizo ipo aliyokuwa akila mhindi, kubeba boksi la dawa, kuvusha watu kwenye mafuriko na kulenga shabaha kwa kutumia bunduki aina ya SMG.
Watangazaji waliokamatwa na baadaye kuachiwa ni Neema Msafiri na Edwin Dugange wanaotangaza kipindi cha ‘Morning talk’.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na uongozi wa redio hiyo zilidai kuwa Kasesela aliambatana na maofisa kadhaa wa polisi wakati alipofika kituoni hapo kabla ya kuamuru watangazaji hao kukamatwa.
Ilidaiwa kuwa mmoja wa watangazaji hao aliigiza sauti ya Kasesela ikieleza mipango yake wilayani hapo.
Hata hivyo, watangazaji hao baada ya muda mfupi waliufahamisha umma kuwa kipengele hicho kilikuwa ni mahsusi kwa ajili ya kuadhimisha siku ya wajinga duniani na waliwataka radhi.
Lakini saa chache baada ya tukio hilo, Kasesela alifika kwenye ofisi za redio hiyo na kuagiza kutiwa nguvuni watangazaji hao ambao waliachiwa baadaye.
Mkuu wa vipindi wa Ebony Fm, Edo Bashir alisema: “Tunashukuru waliachiwa, hivyo tunaendelea kutekeleza majukumu yetu kama kawaida.”
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, Frank Leonard alilaani tukio hilo akisema limeidhalilisha taaluma ya habari.
Alisema watangazaji hao waliitumia siku ya wajinga inayotambulika kimataifa hivyo ilimpasa Kasesela kutumia hekima kabla ya kuwakamata.
“Haya yote ni kutokana na sheria kandamizi zilizopo ikiwamo ya mkuu wa wilaya kuruhusiwa kumuweka ndani mtu yeyote kwa saa 24. Kitendo hiki kimeidhalilisha redio, watangazaji na sisi waandishi wote wa Iringa,” alisema.
Alisema wanahabari wa mkoa huo watashindwa kutekeleza wajibu wao na kuzitumia siku nyingine ipasavyo kutokana na vitisho vya aina hiyo.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Kasesela alisema aliwakamata kwa kosa la kuiga sauti yake jambo lililozua hofu kwa wakazi wa Iringa.
“Waliigiza sauti yangu kwa madai ya kuwa wanasherehekea sikukuu ya wajinga, lakini walikuwa wanatoa ofa nyingi na wananchi wakaanza kuhaha,” alisema.
Alisema wapo waliompigia simu na kutaka kujua ahadi hizo alizotaja redioni jambo ambalo alisema ni kutumia vibaya jina lake.
Hata hivyo, alikana kuwaweka rumande kwa saa mbili, akidai kwamba waliandikisha maelezo polisi na kuruhusiwa kuondoka.
0 comments:
Post a Comment