CHAMA cha ACT-Wazalendo Wilaya ya Shinyanga Mjini kimetamba kuwa kwenye
uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ndicho kitakuwa mpinzani mkubwa wa CCM
badala ya Chadema.
Katibu wa ACT-Wazalendo, Wilaya ya Shinyanga, Melkyoli Sebastian alisema
hayo baada ya kumuingiza kwenye chama hicho, kada wa Chadema, Ibrahimu
Mbogoma.
Mbogoma alikuwa mwenyekiti wa baraza la wazee kata ya Masekelo manispaa ya Shinyanga.
Sebastian alisema chama chao kimeanza kuaminiwa na wananchi kutokana na
sera zake za kiujamaa ambazo zimelenga kumkomboa mwananchi wa hali ya
chini bila ya kubagua dini, kabila wala rangi.
Alisema kutokana na sera hizo, ndiyo maana wanachama wa Chadema wameanza
kujiunga na chama chao baada ya kusoma alama za nyakati.
“Kujiunga kwa kada huyo aliyekuwa Chadema ni salamu tosha kuwa Chadema
inaelekea kufa kiupinzani, nina imani wapo wanachama wengi wa vyama vya
upinzani watakuja kujiunga na ACT Wazalendo.
"Sisi tunawakaribisha waje kwa wingi ili tukijenge chama kuelekea Ikulu 2020,” alisema Sebastian.
Akieleza sababu za kuhama Chadema, Mbogoma, alisema ameamua hivyo
kutokana na kuchoshwa na migogoro ndani ya Chadema pamoja na kuongozwa
na viongozi wasiojua majukumu yao.
Mbogoma alisema tangu alipojiunga na Chadema mwaka 2010 hajaona
mafanikio yoyote licha ya kushika nyadhifa mbalimbali. Alisema amekuwa
akikumbana na migogoro ya mara kwa mara. Alisema anaamini ACT-Wazalendo
ndicho kitaipindua CCM.
Katibu wa Chadema wilaya ya Shinyanga Mjini, George Kitalama alisema
alikuwa hajapata taarifa rasmi za kiofisi za kuhama kwa mwanachama wake
huyo.
Hata hivyo, alisema kila mtu ana haki ya kwenda kujiunga kwenye chama anachokitaka kwa mujibu wa Sheria za nchi.
0 comments:
Post a Comment